The House of Favourite Newspapers

Raia 7 wa Kigeni Mbaroni kwa Utapeli Mtandaoni -Video

0

JESHI la Polisi nchini  leo, Septemba 12, 2020,  limesema linawashikilia watu saba ambao ni raia wa nchi za kigeni kutokana na tuhuma za utapeli wa kwenye mitandao.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, raia hao ni kutoka nchi za Nigeria, Liberia, Congo DR, Afrika Kusini na India ambao majina yao ni: Adewale Nuren Oyedes (34), Ibrahim Darbey (44), Cream Milton Elias (38), Basube Dominic (44), Prince Tito (46), Sibongile Arhur (44). Baljit Singh (28).

 

Miongoni mwa vitu walivyokamatwa navyo ni Sh. milioni 10, gari, runinga mbili na magodoro, na taarifa hiyo imeongeza kwamba polisi wanachunguza kubaini iwapo watuhumiwa hao walishirikiana na Watanzania katika vitendo hivyo.

 

Watuhumiwa watafikiwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.

 

Wakati huohuo, taarifa hiyo inasema watu wawili wanashikiliwa kwa kujifanya maofisa usalama wa taifa, polisi na wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kisha kutapeli wananchi na kujipatia jumla ya Sh. milioni 35.

 

Watu hao ni Patrick Tarimo (32) na Castory Wambura (57) ambao watafikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA MAKOSA MBALIMBALI YA JINAI.​

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawashikilia watu 09 kwa tuhuma mbalimbali za uhalifu hapa Jijini DSM.

Kukamatwa kwa raia 07 wa mataifa mbalimbali ya kigeni kwa tuhuma za kufanya uhalifu kwa njia mtandao (CYBER CRIME).

Watuhumiwa hao ni; –

1. ADEWALE NUREN OYEDES (34) Raia wa Nigeria

2. IBRAHIM DARBEY (44) Raia wa Liberia

3. CREAM MILTON ELIAS (38) Raia wa Liberia

4. BASUBE DOMINIC (44), Raia wa DRC

5. PRINCE TITO (46), Raia wa Liberia.

6. SIBONGILE ARHUR (44), Raia wa Afrika Kusini.

7.BALJIT SINGH (28), Raia wa India.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam katika kipindi cha mwezi Agosti na Septemba 2020 katika maeneo mbalimbali ya Jiji limefanya msako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hawa ambao wamekuwa wakifanya utapeli na wizi kwa njia ya mtandao.

Baada ya mahojiano watuhumiwa walikiri kujipatia pesa kiasi cha Tsh 10,000,000/= kwa njia ya udanganyifu kupitia mtandao na baadhi ya pesa hizo zilitumika kuanzisha duka la vinywaji vya pombe kali eneo la Tangi bovu Mbezi beach, walinunua gari Toyota aina ya MARK X, Televisheni mbili na magodoro.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum linaedelea na uchunguzi ili kubaini Watanzania wanaoshirikiana nao.

Watuhumiwa wote 07 watafikishwa mahakamani hivi karibuni.

KUKAMATWA KWA WATUMIWA WAWILI WANAOJIFANYA MAOFISA USALAMA WA TAIFA NA POLISI.​

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kujifanya maofisa usalama wa Taifa, Polisi na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA)

 

Watuhumiwa hao ni: –

1. PATRICK TARIMO (32), Mkazi wa Mwenge, anajitambulisha kama afisa usalama wa Taifa.

2. CASTORY WAMBURA (57), Mkazi wa Kibamba, anajitambulisha kama ofisa wa Polisi.

 

Watuhumiwa wote wawili wamekuwa wakitapeli raia wema kwa kujifanya waajiriwa wa Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi.

Mtuhumiwa Patrick Tarimo mnamo tarehe 10/08/2020 alijipatia kiasi cha Tsh 20,000,000/= kutoka kwa raia wa kigeni ambapo alimkamata na kujitambulisha kuwa yeye ni afisa usalama wa Taifa na kufanikiwa kujipatia kiasi hicho.

Mtuhumiwa Castory Wambura mnamo tarehe 21/08/2020 alitapeli kiasi cha Tsh 15,000,000/= kutoka kwa wafanyabiashara watano wa kariakoo, ambapo alijitambulisha kuwa yeye ofisa wa Polisi na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA)

Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

SACP- LAZARO B. MAMBOSASA,

KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM,

DAR ES SALAAM.

Leave A Reply