The House of Favourite Newspapers

Raia Wageni Wakamatwa Airport Wakitorosha Mamilion ya Fedha

ABIRIA wawili Raia wa Sudan Kusini na Syria jana wamekamatwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) wakisafirisha fedha taslim dola 70,000 za Kimarekani sawa na shilingi milioni 156 za Kitanzania na paundi 3410 za Sudan bila kufuata taratibu.

 

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria la JNIA, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi, Barnabas Mwakalukwa alimtaja Raia wa Sudan Kusini Bi. Nada Zaelnoon Ahamed (38) mwenye hati ya kusafiria namba P01563534 amekamatwa saa 10:00 jioni akiwa eneo la ukaguzi wakati akiingia ndani tayari kusafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ 485) akielekea Nairobi.

 

 

Hatahivyo, Afande Mwakalukwa amesema abiria huyo amekamatwa na dola 60,000 za Kimarekani na paundi za Sudan 3410, ambazo zote kwa pamoja alishindwa kutoa taarifa ya fedha alizokutwa nazo kwa mujibu wa sheria ya utakatishaji fedha ya mwaka 2006 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.

 

Pia alimtaja Bw. Mohamed Belal (31), Raia wa Syria mwenye hati ya kusafiria namba 003-16L096876 aliyekuwa akisafiri kwa ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia (ET 864) kuelekea Syria kupitia Addis Ababa amekamatwa na dola za kimarekani 10,000 sawa na Tsh. milioni 20 za Kitanzania, ambazo naye alishindwa kuzitolea taarifa.

 

“Watuhumiwa wote wawili wamezuiwa na hawawezi kuendelea na safari zao kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hatua za kisheria zilizopo,” amesema Afande Mwakalukwa.

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela amewapongeza maafisa usalama wa JNIA kwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha wasafiri, wadau na maeneo yote ya viwanja vya ndege yanabaki salama na vitendo vya kiuhalifu havina nafasi katika viwanja hivyo.

 

Bw. Mayongela amesema pamoja na watumishi hao kufanya kazi katika wakati mgumu kutokana na baadhi ya abiria kuwa watata kila wanapotaka kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kanuni.

 

Ametoa wito kwa wadau, wasafiri na wafanyakazi wote kushirikiana na maafisa usalama, vyombo vya ulinzi na usalama katika kutoa taarifa stahiki ili vitendo vya kiuhalifu kama hivi visipate nafasi kwenye viwanja vya ndege kwani ndio vinatoa taswira ya nchi.

MAAJABU!! Nyangumi Mkubwa Anasa Baharini

Comments are closed.