Rais al-Bashir Mahakamani, Akiri Kupokea Rushwa ya USD 90m

Upande wa mashitaka katika kesi ya ufisadi inayomkabili rais wa zamani wa Sudan, Omar al-Bashir, umeiambia mahakama mjini Khartoum leo kuwa kiongozi huyo amekiri kupokea dola milioni 90 taslimu kutoka kwa Ufalme wa Saudia Arabia.

 

Brigadia Ahmed Ali alisema Bashir alimuambia kuwa malipo ya mwisho yaliwasilishwa kwake na baadhi ya wajumbe wa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman.

 

Afisa huyo wa upelelezi aliiambia mahakama kuwa walikuta kiasi cha euro milioni saba pamoja na kiwango kidogo cha dola za Kimarekani na paundi za Sudan kwenye makaazi ya Bashir, ambaye alisema zilikuwa sehemu ya kitita cha dola milioni 25 ambazo Bin Salman alimpa kwa matumizi yaliyo nje ya bajeti.

 

Bashir alisema alikuwa amepokea malipo mara mbili ya dola milioni 35 na milioni 30 kutoka kwa Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia aliyefariki dunia mwaka 2015. Bashir ambaye aliitawala Sudan kwa miaka 30, alifikishwa mahakamani leo akisindikizwa na msafara mkubwa wa kijeshi.


Loading...

Toa comment