The House of Favourite Newspapers

RAIS ALIYEMVAA REFA NA BASTOLA ASABABISHA HAYA

BAO lililokataliwa dakika za mwishoni katika ligi ya soka nchini Ugiriki Jumapili iliyopita, lilimfanya rais wa klabu ya PAOK, Ivan Savvidis, kuingia uwanjani akiwa na bastola yake iliyokuwa kwenye kifuko chake kiunoni, kwenda kuzozana na mwamuzi, Giorgos Kominis, aliyelikataa bao la Fernando Varella alilofunga katika dakika ya 98 dhidi ya timu ya AEK Athens wakati timu hizo zilikuwa suluhu.

 

Pamoja na kwamba Savvidis hakuitoa bastola hiyo, kocha wa AEK, Manolo Jimenez, alidai kwamba Sayyidis alimtishia mwamuzi huyo kwa maneno kwamba “umekwisha, wewe si mwamuzi tena”.
Hata hivyo, bao hilo hatimaye liliruhusiwa baada ya saa mbili kupita, kwa mujibu wa matangazo ya televisheni ya taifa, na kuwaacha mashabiki wa klabu ya PAOK waliofika katika Uwanja wa Toumba, wasiwe na uhakika wa matokeo ya mwisho.

Wakati huohuo, tovuti rasmi ya ligi hiyo bado inaonyesha kwamba mechi hiyo ilitoka suluhu.
Akizungumza na kituo cha radio cha Cadena SER, Jimenez alisema: “Ilionekana kwamba (Savvidis) alikuwa anaelekeza mkono wake kiunoni kwani alikuwa na bunduki. Alimtishia mwamuzi mbele yangu. Kwa mujibu wa mkalimani, alimwambia kwamba ‘umekwisha, wewe si mwamuzi tena’. Nimeshangaa, sikuelewa kitendo hicho. Ni aina ya vitu ambavyo unategemea kuviona kwenye sinema.”

 

Kwa upande wake, klabu ya PAOK ilisema katika taarifa: “Baada ya kile kilichotokea leo, mwenyekiti wa PAOK, Ivan Savvidis, anatayarisha kila kinachotakiwa ili kuilinda timu dhidi ya vitisho na mashambulizi ambayo yamekuwa yakielekezwa dhidi yake. Tutatoa matangazo kuhusiana na hali hiyo hivi karibuni.”
Wakati ligi ikiendelea,

 

PAOK ilipoteza pointi tatu ilizonyang’anywa muda mfupi kabla ya mechi hiyo kutokana na mashabiki wake kufanya vurugu wakati wa mechi dhidi ya Olympiakos iliyovunjika Februari baada ya meneja wake kupigwa na furushi la karatasi kichwani.

 

“Tabia hizi zinahitaji maamuzi magumu,” alisema Waziri wa Michezo wa Ugiriki, Georgis Vassiliadis, katika taarifa iliyotolewa na kuongeza: “Hatutakubali mtu yeyote kutuzuia katika dhamiri hii, pamoja na kwamba maamuzi magumu yanahitaji kuwasiliana na shirikisho la soka la Ulaya (UEFA)”.

Mambosasa: Abdul Nondo Alikwenda Iringa kwa Mpenzi Wake

Comments are closed.