ZAMBIA inaomboleza kifo cha samaki wake mkubwa katika Chuo Kikuu cha Umma cha Copperbelt (CBU). Samaki huyo aliyejulikana kama ameombolezwa na Rais Edgar Lungu na kiongozi wa upinzani Hakainde Hichilema.
Neno Mafishi limekuwa likisambaa kwa kasi katika mtandao wa Twitter nchini Zambia kufuatia kifo cha samaki huyo Jumatatu usiku.
Samaki huyo alikuwa akiishi katika kidimbwi cha chuo kikuu na baadhi ya wanafunzi walikuwa wakimtembelea kabla ya kufanya mtihani ili kuomba wapite. Wanafunzi wengine wanasema aliwasaidia kujiondolea msongo wa mawazo.
Rais Lungu alitumia nukuu ya Mahatma Gandhi kumuomboleza samaki huyo kwa kuandika: ”Ukuu wa taifa na maendeleo ya maadili yake yanaweza kuhukumiwa kutokana na jinsi unavyowatendea wanyama wake.”
Bwana Hichilema aliandika: “Tunaungana na jamii ya wanafunzi wa sasa na wa zamani wa chuo kikuu cha CBU, kufuatia kifo chasamaki wao Mafishi.”
Samaki huyo alikuwa sehemu ya mpango wa turathi ya viumbe wa majini na anasemekana ameishi ndani ya kidimbwi cha chuo hicho kwa karibu miaka saba, kwa mujibu wa kituo binafsi cha televisheni, Diamond.