The House of Favourite Newspapers

Rais Bush Amtapikia Waziri Mkuu wa Japan

0

George-Bush-Images-HDRais wa 41 wa Marekani, George H.W Bush.

\Hebu vuta picha, mheshimiwa rais yupo ukumbini akipata chakula cha usiku na watu wengine mashuhuri lakini ghafla anaanza kutapika na kuwachafua watu aliokaa nao jirani! Unadhani haiwezi kutokea? Basi kwa taarifa yako tukio kama hilo limewahi kutokea.

Kiichi MiyazawaWaziri Mkuu wa Japan wa zamani, Kiichi Miyazawa

Rais wa 41 wa Marekani, George H.W Bush amewahi kukumbwa na tukio lisilo la kawaida la kutapika wakati wa chakula cha usiku nchini Japan.

Ilikuwaje? Januari 8, 1992, Bush alialikwa na Waziri Mkuu wa Japan (kwa wakati huo), Kiichi Miyazawa katika chakula cha usiku wakati akiwa ziarani nchini humo. Bush akaukubali mwaliko huo ambapo alijumuika na viongozi wengine mashuhuri wapatao 100 usiku huo.

Wakati wakiendelea kupata msosi, Bush akiwa amekaa jirani kabisa na mwenyeji wake, Kiichi, ghafla alianza kujisikia vibaya, kichefuchefu kikapamba moto. Akiwa bado hajui afanye nini, Bush alianza kutapika mfululizo, matapishi yakamrukia mwenyeji wake na kusababisha hali ya sintofahamu.

Ilibidi mkewe ambaye alikuwa ameambatana naye kwenye ziara hiyo, Barbara Bush afanye kazi ya ziada kumsitiri mumewe asizidi kuumbuka. Walinzi wake wakawahi kumuinua na kumtoa eneo hilo huku wengine wakifanya kazi ya kufuta matapishi na kumsafisha Kiichi aliyekuwa amelowa matapishi.

Muda mfupi baadaye, taarifa za tukio hilo zilisambaa kwa kasi ya kimbunga dunia nzima, ikabidi msemaji wa ikulu kwa wakati huo, Marlin Fitzwater atoe ufafanuzi kwamba Bush alishikwa na mafua makali (flu) yaliyosababisha hali hiyo.

“Rais naye ni binadamu kama sisi, huwa anaugua,” alikaririwa msemaji huyo. Hata hivyo, kauli hiyo haikuzuia watu kuendelea kulizungumzia tukio hilo.

Usiku huohuo, mwanaume mmoja, James Edward Smith, alipiga simu kwenye kituo cha runinga cha CNN akijifanya ni daktari wa rais, akawaeleza kwamba Bush amefariki dunia baada ya kuendelea kutapika kwa muda mrefu.

Almanusra CNN wairushe habari hiyo kama ‘breaking news’ kabla ya muda mfupi baadaye kugundua kwamba haikuwa na ukweli wowote.

Kwa kipindi kirefu baadaye, wachekeshaji wengi wa ndani na nje ya Marekani waliendelea kulirudia tukio hilo kwa namna ya kuchekesha na kuwavunja wengi mbavu.

Leave A Reply