The House of Favourite Newspapers

Trump, Melania Wawatembelea Ghafla Wanajeshi wa Marekani Nchini Iraq

 

RAIS wa Marekani, Donald Trump na mke wake Melania Trump, wamefanya ziara ya ghafla ya Krismasi ya kuwatembelea wanajeshi wa Marekani walioko nchini Iraq.

 

Walisafiri kwenda huko usiku wa siku ya Krismasi kuwashukuru wanajeshi hao kwa huduma yao, mafanikio na kujitolea kwa mujibu wa White house.

 

Trump alisema Marekani haina mpango wa kuondoka nchini Iraq.

Ziara hiyo inafanyika siku chache baada ya Waziri wa Ulinzi, Jim Mattis, kujiuzulu kufuatia mgawanyiko wa sera za Trump eneo hilo.

 

Marekani ina wanajeshi 5,000 nchini Iraq kuunga mkono serikali katika vita dhidi ya kundi la Islamic State.

Hata hivyo mkutano uliopangwa kati ya Trump na Waziri Mkuu wa Iraq, Adel Abdul Mahdi, ulifutwa. Ofisi ya Mahdi ilisema hiyo ni kwa sababu ya kutokubaliana jinsi mkutano huo ungefanyika.

 

Mazungumzo kwa njia ya simu kati ya viongozi hao badala yake yalifanyika na Ikulu ya Marekani (White House) inasema Mahdi alikubali mwaliko kwa kuzuru Marekani.

 

 

Trump, mke wake na mshauri wa usalama wa kitaifa, John Bolton, walisafiri wakitumia ndege ya Air Force One kwenda kambi ya jeshi ya al-Asad magharibi mwa mji mkuu Baghdad kukutana na wanajeshi.

 

Hiyo ni ziara yake ya kwanza ya aina hiyo eneo hilo.

 

Wakati wa ziara hiyo alipata mapokezi  mazuri kutoka kwa wanajeshi wakati akiingia ukumbi wa maakuli na kutembea akiwasalimia wanajeshi na kupiga picha nao.

 

Alisema sababu ya ziara hiyo ni kuwashukuru wanajeshi kwa kusaidia kuwashinda Islamic State.

Comments are closed.