Rais George Washington; aliapishwa akiwa na jino 1
Unaweza kudhani kwamba ni stori za kizushi lakini ni ukweli mtupu! Rais wa kwanza wa Marekani, George Washington, wakati anaapishwa kuwa rais wa taifa hilo kubwa duniani, alikuwa na jino moja tu halisi mdomoni, mengine yote yalikuwa ya bandia.
Washington aliyetawala kuanzia Aprili 30, 1789 hadi Machi 4, 1797, enzi za ujana wake alikuwa na tatizo sugu la meno kuoza, kuuma na kung’oka na inaelezwa kwamba akiwa na umri wa miaka 24 tu, tayari alishaanza kung’oa meno ambayo yalikuwa yakimsumbua na kumsababishia maumivu makali, hasa nyakati za usiku.
Licha ya kuajiri wataalam wengi kwa ajili ya kumtibu tatizo lake la meno, wakiwemo Dr. John Baker, Jean-Pierre Le Mayeur na Dr. John Greenwood, yaliendelea kupukutika mdomoni na mpaka anachaguliwa kuwa rais, alikuwa amebakiza moja tu ambalo nalo halikudumu, akawa kibogoyo.
Hata hivyo, licha ya tatizo lake hilo ni watu wachache sana waliokuwa wanajua kwamba Baba wa Taifa la Marekani hakuwa na meno. Madaktari wa meno kutoka sehemu mbalimbali nchini humo, walifanya kazi ya ziada ya kumrejeshea meno rais wao.
Awali, Washington aliyekulia kwenye familia ya kitajiri, aliwekewa meno halisi ya binadamu ambayo inaelezwa kwamba alikuwa akiyanunua kutoka kwa watumwa lakini nayo yalionesha kutomsaidia.
Badala yake, akaanza kuchongewa meno bandia kwa kutumia pembe za ndovu, faru na wanyama wengine ambayo kwa kuyatazama, usingeweza kudhani kwamba ni meno bandia. Akawa anayavaa na kufanya iwe vigumu kwa watu wengi kugundua tatizo lake.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa meno ya bandia yalikuwa yakimsababishia maumivu makali mdomoni na kumfanya ashindwe kuzungumza vizuri wala kula vizuri.
Inazidi kuelezwa kwamba meno hayo ya bandia pia yalikuwa yakisababisha mwonekano wake ubadilike mara kwa mara, hasa eneo la mdomoni ambapo muda mwingine yalikuwa yakipinda na kumfanya aonekane kuwa na mdomo mkubwa au uliopinda.
Wapo wataalam walioeleza kwamba matatizo hayo ya meno ya Washington, yalisababishwa na kutozingatia mlo kamili, maradhi ya mara kwa mara na matatizo ya vinasaba. Hata hivyo, wengine wanaeleza kwamba kuharibika kwa meno ya Washington, kulisababishwa zaidi na mercury oxide aliyokuwa anapewa kutibu magonjwa yaliyokuwa yakimsumbua mara kwa mara.
Hata baada ya kifo chake, meno ya bandia yaliyokuwa yakitumiwa na Washington, yameendelea kuhifadhiwa kwenye makumbusho nchini humo na kwenye vyuo mbalimbali, kikiwemo New York Academy of Medicine na Mount Vernon