The House of Favourite Newspapers

RAIS JPM AMEMPONZA MAKONDA?

KWA waliosoma Biblia, kisa cha Yusufu na baba yake, Yakobo hakiwezi kuwa kigeni. Yusufu alipendwa mno na baba yake, alikuwa ni mtoto wa uzeeni kwa Yakobo, aliyempata kwa mkewe wa pekee, Raheli. Watoto 10 waliotangulia kuzaliwa na Yakobo walimchukia Yusufu kutokana na mapenzi aliyokuwa akioneshwa waziwazi na baba yake, akachukiwa bila sababu.

MAISHA YA MAKONDA NA UONGOZI WA JPM

Japokuwa kisa hiki hakina uhalisia wa moja kwa moja na maisha halisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’, lakini kwa yanayotokea, yanaakisi mfano huo kutoka katika Biblia.

Upendo wa Yakobo kwa Yusufu haukuwa na maana mbaya, yalikuwa ni maono ya ‘Ki-mungu’ maana Yusufu alikuja kuwa msaada mkubwa kwa taifa la Misri. Yusufu alikuwa na kipawa cha aina yake cha kuweza kutambua mambo yajayo kupitia ndoto, jambo hilo halikuwapendeza ndugu zake hadi kufikia shauri la kumuua.

Rais Magufuli amekuwa akiguswa na utendaji kazi wa Makonda na kutoona tatizo kumpongeza hadharani, hicho ndicho kinachomponza Makonda, nitafafanua. Mathalan, Machi 2017 Rais Magufuli alipokuwa kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za juu (fly-over) Ubungo, alimtaka Makonda achape kazi bila kusikiliza maneno ya watu.

“Mimi ni Rais ninayejiamini, siwezi kupangiwa, hata siku ya kuchukua fomu nilienda mwenyewe, nitaamua mwenyewe nani akae wapi, kwa hiyo Makonda wewe chapa kazi, nasema chapa kazi. Najua wamenielewa. Kuandikwa kwenye mitandao siyo tija kwangu, hata mimi naandikwa kwenye mitandao, kwa hiyo nijiuzulu urais?” Alisema Rais Magufuli siku hiyo.

Kwa namna moja au nyingine, kauli hiyo ya Rais ilionekana kuchochea zaidi watu kumchukia Makonda kwa chuki tu na wivu usiokuwa na kichwa wala miguu kama ilivyokuwa kwa ndugu zake Yusufu. Asingemtetea hadharani, vurugu mitandaoni pengine zisingekuwa kubwa kiasi hicho.

Lakini kwa sababu tu anaonekana kumtetea, wanahisi anampenda sana na ndiyo shinikizo la kumtaka Rais amtumbue Makonda limekuwa likikolezwa siku hadi siku. Hili lilionekana dhahiri hata kwa baadhi ya wabunge, walisikika wakipinga juhudi mbalimbali za Makonda na kumshawishi Rais amtumbue.

Mbali na wabunge, wapo pia viongozi wa Serikali ambao walionesha kumpinga Makonda na hiyo ilijidhihirisha pale linapoibuka jambo lolote lenye mlengo hasi kwa Makonda, lilishikiwa bango kwelikweli. Alipoanzisha oparesheni ya kupinga madawa ya kulevya kwa kuwataja hadharani wahusika, kelele zikawa nyingi, kwamba hakufuata sheria, anakurupuka na mambo mengine kadha wa kadha.

Lilipokuja suala la Makonda kuvamia Kituo cha Clouds TV, debe likapigwa kwelikweli kwamba Makonda hafai kuwa kiongozi. Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alikuwa miongoni mwa waendesha kampeni maalum ya ‘kumpiga’ Makonda.

Kutokana na Makonda kuonekana kuingilia uhuru wa habari, kwa kuvamia kituo hicho na askari wenye bunduki ikidaiwa anakwenda kushinikiza kipindi anachokitaka kiruke hewani, watu wengi waliamini kwamba sasa ufalme wa Makonda unafika ukingoni. Waliamini Rais hawezi kumvumilia katika hilo.

Tofauti na matarajio ya wasiompenda Makonda, Oktoba 13, 2017, akiwa kwenye mkutano mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), Rais Magufuli aliwataka wakuu wa mikoa kuiga mfano wa Makonda. Alisema watu wameibua suala la elimu ya Makonda wakati ambao ameanzisha vita ya madawa ya kulevya hivyo hatawasikiliza.

Aliwataka wakuu wengine wa mikoa waige mfano wa Makonda na kwamba kwake yeye hata kama Makonda hajui kusoma na kuandika, lakini kwa vita anayopigana ya madawa ya kulevya, ni mtu bora kuliko hata wale waliosoma.

Rais Magufuli alijaribu kuhoji kwamba katika wenyeviti waliopo kwenye mkutano huo, wapo wasomi, lakini ndiyo haohao ambao Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) imekuwa ikionesha hawapati matokeo mazuri hivyo kikubwa anachokiangalia kwa Makonda ni uzalendo na uchapakazi.

TAFAKARI YANGU

Rais Magufuli kweli amekuwa akionesha mapenzi kwa Makonda kama vile Yakobo alivyomnunulia Yusufu koti zuri tofauti na wenzake, lakini matokeo yake ikawa tatizo kwa Makonda.

Rais amemsifia Makonda pale panapostahili kusifiwa ikiwemo katika suala hilo la vita ya madawa ya kulevya, ujenzi wa madarasa ya shule mbalimbali na ukarabati wa magari ya Polisi, lakini sifa hizo zinageuka kuwa sumu hatari kwa wasiompenda.

Yawezekana asingemsifia, tafsiri ya wale wasiompenda wasingeona wivu, angefanya kazi zake vizuri na pale alipokosea, basi Rais angeweza kumkosoa kaa vile anavyoweza kuwakosoa wateule wake wengine pindi anapoona hawaendi kwenye mstari anaoutaka. Chuki kubwa imejengeka kutokana watu wenye wivu kuumizwa tu na yale ‘mahaba’ ya Rais kwa mteule huyo.

Wanamchukia bila sababu, wanataka kumuangamiza kama vile ndugu zake Yusufu walivyoamua kumuangamiza kwa kumtupa shimoni kisha kuchukua vazi lake na kulipaka damu ya kondoo kumpelekea baba yao kumueleza kwamba Yusufu ameuawa au ameliwa na mnyama mkali.

Tafsiri ya Makonda kuchukiwa, haina tofauti sana na ile ya Yusufu. Yusufu aliwaeleza ndugu zake ndoto iliyoashiria yeye atakuwa mkubwa kuliko wao waliotanguliwa kuzaliwa, hilo halikuwapendeza ndugu zake na hiyo ndiyo inayojidhihirisha hata kwa watu wasiompenda Makonda jinsi wanavyotaka kumuangamiza.

Ndiyo haya tuliyoyasikia juzi katika sakata la makontena, shinikizo limeanza upya na watu wanataka Makonda atumbuliwe!

MAKALA: Erick Evarist, DAR

Comments are closed.