JPM Aagiza Mkuu Shule Iliyoteketea Kagera Aachiwe

SELEMAN ABDUL, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Byamungu Islamic, iliyopo Kyerwa mkoani Kagera, ametetewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba, hakukusudia kuchoma bweni la shule hiyo na kusababisha maafa.

 

Usiku wa kuamkia tarehe 14 Septemba 2020 bweni la shule hiyo liliteketea kwa moto na kusababisha vifo vya wanafunzi 10 na wengine kujeruhiwa. Kutokana na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera lilimtia nguvuni Abdul ili kuendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

 

Leo Jumatano tarehe 16 Septemba 2020, akihutubia mkutano wa kampeni za urais katika viwanja vya Gymkhana, Bukoba mkoani Kagera, ameanza kwa kuwaomba wananchi waliohudhuria mkutano huo kusimama dakika moja kuwaombea wanafunzi hao.

Amesema mkuu wa shule hiyo anaweza kusaidia uchunguzi wa tukio hilo akiwa nje.

 

“Napenda kutumia fursa hii kutokana na msiba uliotupata kule Kyerwa kuzihimiza mamlaka zote husika nchini, Tamisemi na Wizara ya Elimu, kuhakikisha shule zote zinazingatia masuala ya usalama na sheria kabla na hata baada ya kuanzishwa, ili madhara haya ya moto na ajali mbalimbali kwenye shule zetu, yasijirudie.

 

“Ninafahamu mkuu wa shule ameshikiliwa na jeshi la polisi. Mimi ningeomba Jeshi la Polisi wakati wakiendelea kufanya uchunguzi, huyu mkuu wa shule wamuachie, kwa sababu hata akiwa nje ya mahabusu, nina uhakika atendelea kushirikiana na polisi katika kutoa taarifa,” amesema Magufuli.

Amesema, anaamini mkuu huyo wa shule hakuwa tayari kuwachoma watoto hao na kuwa, kuendelea kumweka ndani wakati wa uchunguzi, ni kuendelea kumpa mateso zaidi.

 

“Kwa hiyo Mkuu wa Mkoa (Brigedia Jenerali Marco Gaguti), mimi naomba huyo baba nina uhakika mkuu wa shule hana moyo mbaya hivyo wa kuchoma hawa watu. Yeye alianzisha shule kwa ajili ya kusomesha watoto wetu, naomba awe nje kwa sababu tunamwongezea mateso mengine mbali na mateso ya kupotelewa na wale watoto kumi ambao aliwalea kama watoto wake,” amesema Magufuli.

 
Toa comment