The House of Favourite Newspapers

Rais Magufuli Aagiza Makao Makuu ya TANESCO Kubomolewa

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la juu (Fly Over) eneo la TAZARA jijini Dar es salaam akiwa ameongozana na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda mara tu baada ya kuwasili kutokea kijijini kwake Chato mkoani Geita leo Jumatano Novemba 15, 2017.
Rais Dkt John Pombe Magufuli akizungumza mapema leo mbele ya baadhi ya Wananchi (hawapo pichani) walikuwepo katika eneno hilo, mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Flyover ya Tazara,kushoto ni Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mh.Paul Makonda
Rais  Magufuli akiwa  na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan wakiwa sambamba na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mh.Paul Makonda walipokuwa wakiwasili maeneo ya Ubungo na kuanza kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara za juu za Ubungo ‘Ubungo Interchange’.

Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan wakimsikiliza mmoja wa Wakandarasi wa mradi huo wa ujenzi wa barabara za juu ‘Ubungo Interchange’,mapema leo
Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wananchi mbalimbali waliokuwa wamejitokeza mapema leo
Baadhi ya Wafanyakazi wa mradi huo wakishangilia wakati Rais Dkt John Pombe Magufuli alipokuwa akizungumza nao
Maendeleo ya Ujenzi wa Flyover ya Tazara jijini Dar Es Salaam kama unavyoonekana pichani mapema leo mchama,ambapo Rais Dkt John Pombe Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassani walitembelea na kujionea maendeleo yake,ambapo Mkandarasi wa mradi huo amesema kuwa asilimia 63 ya ujenzi umekamilia na kwamba Flyover hiyo inatarajiwa kufunguliwa Agosti 8,2018 badala ya Desemba 2018.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 15 Novemba 2017, amerejea jijini Dar es salaam akitokea kijijini kwake Chato, mkoani Geita.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dare es salaam, Mhe. Rais amepokelewa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda na viongozi wengine wa mkoa.

Baada ya kutoka Uwanja wa Ndege, Rais Magufuli akiwa ameongozana na Makamu wa Rais pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, amekagua Ujenzi wa Daraja la juu Tazara ( Tazara Fly-Over) na Ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo ( Ubungo Interchange)

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Ubungo, Rais Magufuli amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS  Mkoa wa Dar es salaam Mhandisi Ndyamukama Julius kuvunja sehemu ya jengo la TANESCO na jengo la Wizara ya Maji yaliyopo katika eneo la hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja hilo.

”Sheria ya hifadhi ya barabara katika eneo hilo ni mita tisini kila upande kutoka katikati ya barabara hivyo ni lazima sheria hiyo iheshimiwe ili kuharakisha ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu katika eneo hilo la Ubungo uanafanyika bila vikwazo kwani sheria ni msumeno haina budi kuzingatiwa hata na Serikali yenyewe” amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameiagiza TANROADS kutangaza tenda ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita kumi na sita (16) kutoka eneo linapoishia Daraja la ghorofa tatu katika eneo la Ubungo kuelekea Chalinze ili itanuliwe kwa lengo la kurahisha usafiri katika jiji la Dar es salaam.

Rais Magufuli amewataka Makandarasi wanaojenga Daraja la Tazara na Ubungo kuharakisha ujenzi wa madaraja hayo usiku na mchana ili yaweze kumalizika kwa wakati ama kabla ya muda huo katika kurahisisha maendeleo ya kibiashara katika jiji la Dar es salaam.

”Dar es salaam ni jiji la kibiashara hivyo hakuna budi miundombinu yake ya usafiri iweze kurahisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka ndani ya jiji na nje ya jiji la Dar es salaam” amesema Rais Magufuli.

Mhandisi wa Masuala ya Usalama wa Ujenzi Mhandisi Richard Baruani amemueleza Rais Magufuli kuwa Ujenzi wa Daraja la Tazara umefikia asilimia 64 ambapo Daraja hilo linatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2018.

Kwa upande wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo, Mhandisi Mshauri Reginald Kayanga amesema  ujenzi wake unatarajiwa kuanza rasmi Desemba 2017.

Jaffar Haniu

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

15 Novemba, 2017

Leave A Reply