The House of Favourite Newspapers

MAGUFULI AMZAWADIA PETER TINO KIWANJA, SH. MIL. 5

Mchezaji wa zamani wa timu ya soka ya taifa nchini (Taifa Stars), Peter Tino,  akikamilisha kufungua akaunti ili aweke shilingi milioni tano  jana alizopewa na Rais  John Magufuli kwa kutambua mchango wake kwa  timu hiyo mwaka 1980 ambapo goli lake liliiwezesha Tanzania kufuzu fainali ya michuano ya soka barani Afrika kwa nchi za Afrika  (AFCON). Wanaoshuhudia (nyuma) ni Meneja Biashara wa Tawi la CRDB-Bank  la Azikiwe, George Yatera (kulia) na Ofisa kutoka shirikisho la soka nchini (TFF) John Michael Mashaka. Kushoto ni Ofisa wa Benki hiyo Bi. Gloria Kaale ambaye ndiye aliyemfungulia akaunti nyota huyo wa zamani.
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Peter Tino,  leo amekabidhiwa shilingi milioni 5 alizopewa na Rais  John Magufuli kwa kutambua mchango wake kwa timu hiyo  mwaka 1980 ambayo ilifuzu kuingia fainali za michuano ya soka barani Afrika  (AFCON).

 

 

…Akipongezwa na Magufuli.
Mchezaji Peter Tino ndiye aliyefunga goli lililoiwezesha Tanzania kuingia fainali hizo na tangu mwaka huo wa 1980 Tanzania haikuwahi kufanikiwa tena kuingia hatua hiyo mpaka mwaka 2019 ikiwa ni miaka 39 imepita.
Peter Tino alialikwa Ikulu jijini Dar es Salaam jana tarehe 25 Machi, 2019 wakati Rais Magufuli alipokutana na kuwapongeza wachezaji wa timu ya taifa (Taifa Stars) ambao jana waliifunga timu ya taifa ya Uganda (The Cranes) na kufanikiwa kufuzu kucheza fainali za AFCON 2019 zitakazofanyika baadaye mwezi Juni 2019 huko Misri.
…Akielekezwa na  George Yatera namna na kutumia kadi yake ya ATM baada ya kukamilisha kufungua akaunti. 
Pamoja na kupatiwa shilingi Milioni 5, Peter Tino pia ameunganishwa katika zawadi ya kupatiwa kiwanja jijini Dodoma kwa kila mchezaji wa Taifa Stars iliyotolewa na Rais Magufuli ambapo naye atapatiwa kiwanja cha kujenga nyumba.
Peter Tino ameziweka pesa hizo katika akaunti yake ya Benki ya CRDB-Bank aliyoifungua mara tu baada ya kutoka Ikulu na kukabidhiwa kadi yenye taarifa zake za benki (ATM).
“Hakika Mungu ni mkubwa” amesema Peter Tino baada ya kupokea kadi yake ya Benki kwa Meneja Biashara wa Tawi la CRDB la Azikiwe, George Yatera, akishuhudiwa na ofisa kutoka kutoka TFF, John  Mashaka.
“Hela hii sikuiota hata ndotoni na mradi rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli kanikumbuka hakika sintomwangusha. Yaani nitakwenda kumalizia kibanda changu kule Morogoro, ” alisema mkongwe huyo katika soka.
…Akikabidhiwa kadi yake ya ATM.
Afisa wa Benki hiyo Bi. Gloria Kaale ndiye aliyemsajili mchezaji huyo ambaye wadogo zake, Gebbo Peter na Emma Peter, nao walitikisa anga za soka nchini kwa nyakati tofauti siku za nyuma kabla na wao kustaafu. Familia yao kwa sasa inaishi Morogoro.
Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, ilikuwa ni Agosti 26,1979 wakati timu ya taifa ilipokuwa ikirudiana na timu ya soka ya taifa ya Zambia katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria.   Pambano hilo lilichezwa mjini Ndola.
Mechi hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Taifa Stars kwa vile ilikuwa ikihitaji sare ya aina yoyote ili iweke historia ya kufuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza, tangu ilipoanza kushiriki michuano hiyo mwaka 1968. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa wiki mbili nyuma kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars iliishinda Zambia bao 1-0. Bao hilo lilifungwa na kiungo Mohammed Rishard Adolph.
Ushindi huo ulipatikana kwa mbinde kiasi kwamba mashabiki wengi hawakuwa na imani iwapo Taifa Stars ingeshinda ama kupata sare katika mechi ya marudiano. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani Wazambia walifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika za mapema na kudumu nalo kwa takriban dakika 86.
Zikiwa zimesalia dakika tatu pambano hilo kumalizika, mshambuliaji mrefu mwenye kasi na mashuti makali, Peter Tino alibadili sura ya mchezo na kufanya kile kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa mchezo huo nchini.
Ilipigwa kona kwenye lango la Taifa Stars, kipa Juma Pondamali akaupangua mpira kwa ngumi, ukamkuta kiungo Leodegar Tenga, aliyetoa pasi ndefu kwa kiungo mwenzake, Hussein Ngulungu, ambaye naye alitoa pasi ndefu kwa Tino.
Akiwa amezungukwa na mabeki watatu wa Zambia, Tino alilazimika kupiga hesabu za haraka. Aliwachomoka mbio mabeki nao na kukimbia na mpira kwa kasi. Alipofika nje kidogo ya eneo la hatari la Zambia, alifumua shuti kali la mguu wa kulia, lililompita kipa Shileshi wa Zambia na mpira kutinga wavuni.    Bao hilo lilipatikana baada ya pasi tatu.
Katika mechi hiyo, Taifa Stars iliwakilishwa na kipa Juma Pondamali, mabeki ni Leopard Tasso, Mohammed Kajole/ Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, viungo ni Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu na washambulaji ni Omari Hussein, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally.
Kikosi hicho kilichokuwa chini ya Kocha Slowmir Work kutoka Poland, akisaidiwa na wazawa Joel Bendera na Ray Gama (ambao kwa sasa wote ni marehemu), ndicho kiliiwakilisha Tanzania katika fainali za kombe hilo zilizofanyika nchini Nigeria.
Katika fainali hizo, Taifa Stars ilichapwa mabao 3-1 na wenyeji Nigeria katika mechi ya ufunguzi, ilitoka sare ya mabao 2-2 na Ivory Coast kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na Misri na kutolewa hatua ya makundi.
Hiyo ilikuwa ni miaka 39 iliyopita ambapo hivi sasa, baada ya kuichapa Uganda mabao 3-0 Jumapili, kila Mtanzania ameweka matumaini kwenye kikosi hicho kipya kilicho chini ya kocha kutoka Nigeria, Emmanuel Amunike.

Comments are closed.