JPM Atangaza Kufungua Vyuo, Michezo na Kidato cha Sita – Video
RAIS John Magufuli, ametangaza kuwa kuanzia Juni 1, 2020, michezo, masomo ya kidato cha sita na vyuo vitafunguliwa.
Amesema hayo baada ya kuwaapisha Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Oloyce Mollel, mabalozi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana(Takukuru) Brigedia-Jnerali John Julius Mbungo, na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Delphine Diocles Magere leo Mei 21, Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Amezitaka pia Wizara za Elimu na Fedha kuandaa utaratibu mzuri wa wanafunzi kupata mikopo watakapofika vyuoni na kuandaa pia utaratibu utakaofuata wakati shule za msingi na sekondari zitakapoanza kufanya kazi.
“Tumeamua sisi kama Serikali vyuo vyote vifunguliwe tarehe moja Juni, 2020. Niwaombe sana wizara zinahohusika hasa Wizara ya Elimu na Wizara ya Fedha ambayo inahusika katika kutoa mikopo, zina siku tisa zijiandae ili vyuo vitakapofunguliwa kusiwe na kero zingine.
“Ukianchana vyuo, vijana wa kidato cha sita walio katika mitihani yao nao warudi shuleni kuanzia Juni 1 na wizara ipange mpango mzuri ili wanafunzi wafanye mitihani yao bila kuathiri mpango wa kwenda chuo kikuu”, ameongeza.
Aliongeza kuwa kuanzia Juni Mosi shughuli za michezo, ikiwemo Ligi Kuu ya Soka, Ligi Daraja la Kwanza na Michezo ya Majeshi navyo vitarejea, lakini kwa kuzingatia utaratibu hasa kuhusu mashabiki, utakaotolewa na Wizara ya Afya.
Pamoja na hayo, amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kuhusiana na ugonjwa wa COVID-19 akisema, licha ya kupungua nchini, bado upo, hivyo tahadhari zinapaswa kuendelea.