The House of Favourite Newspapers

Rais Magufuli Azungumza na Rais Museveni wa Uganda

0
3Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifanya Mazungumzo na Rais wa Uganda, Mh. Yoweri Kaguta Museveni, Ikulu ndogo ya Arusha jana.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, amekutana na kufanya Mazungumzo na Rais wa Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, ambapo pamoja na mambo mengine wamekubaliana kujengwa kwa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Bandari ya Tanga nchini Tanzania hadi nchini Uganda.
Rais Museveni alimtembelea Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Arusha jana jioni mara baada ya kuwasili hapa nchini akitokea nchini Uganda, ambapo leo atahudhuria Mkutano Mkuu wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, utakaofanyika katika Hoteli ya Ngurudoto Jijini Arusha.
Akizungumza baada ya viongozi hao kufanya mazungumzo ya faragha, Rais Magufuli alisema wamekubaliana kutekeleza mradi huo wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Tanga hadi Uganda, kwa manufaa ya nchi zote mbili na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Alisema bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,120 na kwamba mradi huo utazalisha ajira za watu zaidi ya 15,000.
Rais Magufuli aliongeza kuwa pamoja na kujengwa kwa bomba la mafuta, pia walizungumzia kuongeza biashara ndani ya nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki, kujenga viwanda na kuzalisha ajira zaidi kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji mali.
Aidha, Rais Magufuli alisema katika Mkutano huu nchi wanachama watajadili maombi ya nchi ya Sudan Kusini kupata uanachama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alibainisha kuwa, kwa Sudan Kusini kuwa mwanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki, itakuwa na uwezo wa kufanya biashara katika eneo lenye takribani watu milioni 150 na hivyo kupata manufaa makubwa zaidi.
Kwa upande wake Rais Yoweri Kaguta Museven pamoja na kuunga mkono yaliyosemwa na Rais Magufuli alimpongeza kwa kasi yake nzuri aliyoanza nayo katika uongozi, na alisema ni matumaini yake kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sasa zitakuwa katika nafasi nzuri ya kwenda kwa kasi ya Rais Magufuli katika maendeleo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
01 Machi, 2016
1 (1)
2
Leave A Reply