The House of Favourite Newspapers

Rais Magufuli kaanza fresh, tukimuangusha itaniuma sana!

maguuliRais Dk. John Pombe Magufuli.

MWEZI mmoja unakatika sasa tangu Dk. John Pombe Magufuli aapishwe na kuanza kazi yake ya urais wa serikali ya awamu ya tano. Ingawa hadi andiko hili linaandikwa alikuwa bado hajataja Baraza lake la Mawaziri, kuna kila dalili kuwa nchi imempata kiongozi iliyokuwa inamhitaji kwa miaka mingi.

Rais ameanza kwa kuhimiza uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma, kupunguza matumizi ya fedha za serikali sambamba na kazi nzito na ngumu ya kushughulika na mafisadi.

Kila anayeitakia mema nchi hii, anampongeza na kumtakia afya njema na ulinzi wa kutosha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Nchi yetu imeoza karibu katika kila sekta inayosimamiwa na serikali, kiasi cha kuonekana kama rais anatakiwa kutembelea ghafla sehemu zote. Ingawa wananchi wana mahitaji mengi muhimu kwa sasa, ni wazi kuwa Magufuli lazima apange vipaumbele vya kuanza navyo, ambavyo ni vya lazima.

Kuna vitu vitatu ambavyo ni lazima mtu avipate kwa wakati kabla ya kufikiria maendeleo. Rais anataka taifa letu lipige hatua ya maendeleo, kutoka hapa tulipo hadi pale mbele. Ili tufike huko, lazima kwanza tuondoe njaa, tutibiwe vyema na watoto wetu wapate elimu bora.

Kwa hiyo, wakati mianya ya mafisadi ikizibwa na fedha stahiki zikikusanywa, wakulima na wafugaji lazima wapewe kipaumbele kwa vitendo. Walime kwa faida ili wajiepushe na njaa wao binafsi na baadaye taifa zima.

Hawa wana vikwazo vingi mno katika utendaji wao wa kazi. Pembejeo zinauzwa kwa bei kubwa, lakini mazao yao yananunuliwa kwa fedha ndogo sana. Kuna ukiritimba mkubwa kukizunguka kilimo. Hapa panahitaji mapinduzi makubwa, hasa kwenye wajibu wa vyombo vya serikali.

Tukimfungua minyororo mkulima, tuhakikishe anapata matibabu ya uhakika na kwa wakati. Hospitali, zahanati na vituo vya afya vipewe uhai, maana kwa sasa, tunazungumzia majengo tu, ambayo yanawanufaisha zaidi madaktari. Dawa hakuna, vifaa tiba hakuna na mbaya zaidi, hata wahudumu wenyewe hawapo!

Uwepo utaratibu wa wazi wa mzunguko wa dawa kutoka Bohari ya Madawa (MSD) hadi vituo vyake. Kuna wizi na kutowajibika kwa hali ya juu kwa maofisa wa serikali katika eneo hili.

Na baada ya kumwondolea njaa na kumpa matibabu ya uhakika Mtanzania huyu wa chini, hasa wa vijijini, sasa tumpe uhakika wa elimu bora kwa mtoto wake kama rais wetu alivyoahidi.

Ingawa serikali imekataza michango, lakini kuna watendaji wengi kule vijijini wataungana na walimu wasio waaminifu, watatunga michango ya uongo na kweli.

Hawa wadhibitiwe na wapewe adhabu za mfano ili kukomesha tabia hii. Mishahara ya walimu iangaliwe upya kwa maana ya kuboreshwa ili kuwapa morali ya kazi na jambo hili lifanyike mara kwa mara kadiri uchumi utakavyokuwa ukiimarika.

Vitu hivi vitatu vikipatikana ni rahisi kufikiria maendeleo na hata wananchi wenyewe wataelewa. Maana kujenga barabara za juu, kuwa na ndege, treni na mabasi ya kifahari hakuwezi kutoa ishara ya taifa kuendelea kama wananchi wa ngazi ya chini wanakosa huduma zile muhimu.

Bei za pembejeo zinaweza kupungua kwa kiwango kikubwa na ‘maushuru’ ya ukandamizaji yanaweza kuondolewa, kwa sababu tumethibitisha taifa linapoteza fedha nyingi kwa mambo yasiyo na tija. Fedha hizi zinaweza pia kununua madawa na kugharamia elimu.

Kitu cha msingi ni kwa wananchi wa ngazi zote, hasa watendaji wa umma kutomuangusha Rais Magufuli, ikiwa hivyo nitaumia sana.

Tumuunge mkono kwa vitendo. Tukiwabana mafisadi, vyanzo vyetu vya mapato vikatumika vizuri, hatuna sababu ya kuombaomba!

Comments are closed.