Rais Morsi Azikwa Saa Chache Baada ya Kufariki Dunia

RAIS  wa zamani wa Misri, Mohamed Morsi, amezikwa saa chache baada ya kufariki dunia akiwa mahakamani siku ya Jumatatu. Wakili wake ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kiongozi huyo wa zamani alizikwa Mashariki mwa jiji la Cairo asubuhi ya Jumanne familia yake ikiwepo

 

Morsi, aliyekuwa na miaka 67, alikuwa kizuizini tangu alipoondolewa madarakani mwaka 2013.

Makundi ya watetezi wa haki za binaadamu, ambayo yalikosoa mazingira ambayo Morsi aliwekwa, yametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu kifo chake.

Familia yake na wanaharakati wamezungumzia kifo chake na muda ambao aliwekwa katika seli ya peke yake, akizuiwa kutembelewa na wanasheria na familia yake.

 

Mtoto wake, Abdullah Mohamed Morsi, ameliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters siku ya Jumatatu kuwa mamlaka za Misri ziliikatalia familia yake kufanya maziko katika mji yalipo makazi yake.

Kiongozi  huyo wa juu wa zamani wa kundi lililopigwa marufuku nchini humo, Muslim Brotherhood,  alikuwa kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia mwaka 2012.

Aliondolewa na kushikiliwa baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka mmoja baadaye baada ya kufanyika maandamano makubwa kupinga utawala wake.

Abdul Fattah al-Sisi, kiongozi wa zamani wa kijeshi, amekuwa madarakani tangu mwaka 2014.

 

Baada ya kuondolewa madarakani, mamlaka zilipambana na wafuasi wake na wapinzani wengine, na kukamata maelfu ya watu.

Muslim Brotherhood na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, mshirika wa karibu wa Morsi ni miongoni mwa walioshutumu utawala wa Misri kuhusu kifo cha Morsi.

 

Kulitokea nini Mahakamani?

Morsi alikuwa mjini Cairo siku ya Jumatatu kwa shutuma za kufanya vitendo vya kijasusi  na mawasiliano na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Kipalestina, Hamas.

Maofisa wanasema aliomba kuzungumza mahakamani na kuongea kwa dakika tano kutoka kwenye kizimba kilichokuwa na kioo ambacho alikuwamo ndani yake na washtakiwa wengine.

Dakika chache baadaye alizimia wakati wa mapumziko mahakamani hapo.

 

”Alipelekwa hospitali ambapo alithibitishwa kupoteza maisha,”taarifa ya mwendesha mashtaka ilieleza.

 

Watu wanazungumza nini baada ya kifo chake ?

”Kifo cha rais wa zamani, Morsi kimetokea kutokana na kutendewa isivyo haki na serikali, kuwekwa katika gereza la peke yake, ambapo  alipatiwa huduma mbovu za matibabu, kumzuia kuonana na familia yake na mawakili wake,” alisema Bi Whitson kwenye taarifa yake.

 

Shirika la Amnesty International pia limetaka uchunguzi ufanyike kuhusu kifo chake.

Shirika limesema Morsi alikuwa akiruhusiwa kutembelewa mara tatu tu kwa kipindi cha takribani miaka sita na hakuruhusiwa kuonana na mawakili wake wala daktari.

Mfalme wa Qatar,Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, mshirika mwingine wa Morsi ameeleza masikitiko yake kutokana na kifo chake.

 

Mbunge wa nchini Uingereza, Crispin Blunt, aliyeongoza jopo la wanasiasa na kutoa tahadhari kuhusu aliyokuwa anatendewa  Morsi mwaka 2018, ametaka ufanyike ”uchunguzi huru kimataifa”.

Tawi la kisiasa la kundi la Muslim Brotherhood, chama cha Freedom and Justice, vimesema kuwa kifo cha Morsi ni ”mauaji”.

Rais Erdogan wa Uturuki amewashutumu ”wakandamizaji” wa Misri kwa kifo chake na kumuelezea Morsi kuwa shahidi.

 

Morsi ni nani?

Mohammed Morsi alizaliwa katika kijiji cha El-Awwadh katika jimbo lililopo kwenye  kingo za Mto Nile huko  Sharqiya mwaka 1951.

Alisomea Uhandisi katika chuo Kikuu cha Cairo katika miaka ya 70 kabla ya kuhamia nchini Marekani ambapo alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uhandisi.

 

 


Loading...

Toa comment