The House of Favourite Newspapers

Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi Afungua Tawi la Benki ya CRDB Wete

0
Rais Mwinyi akigawa pikipiki zilizotolewa na Benki ya CRDB

Rais Dkt Hussein Mwinyi amezindua tawi jipya la Benki ya CRDB na kukabidhi pikipiki na boti za uvuvi na kilimo Ili kuwashirikisha wananchi wengi kuujenga uchumi wa visiwa hivi.

 

Rais alikabidhi jumla ya pikipiki 272 na boti 94 zitakazosaidia kuimarisha shughuli za vijana na wanawake ambazo ni mkopo uliotolewa na Benki ya CRDB.

 

“Tuliahidi sasa tunatekeleza. Mtakumbuka siku chache baada ya kuapishwa kuingia madarakani niliziomba taasisi za fedha kushirikiana na Serikali kufanikisha utekelezaji wa ahadi nilizozitoa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu. Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele katika hili na leo tumeanza na vijana pamoja na, wavuvi na wakulima wa mwani,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa CRDGB Pemba

Dkt Mwinyi alizindua mikopo hiyo kwenye ufunguzi wa tawi la Benki ya CRDB lililopo katika Mtaa wa Sunda, Barabara ya Mtemani akiwahimiza wananchi kuzitumia huduma zake kufanikisha shughuli zao za kiuchumi.

 

“Tawi hili linatoa huduma za benki kwa masharti ya Kiislam na yale ya kawaida. Serikali kwa kushirikiana na wadau imedhamiria kuwawezesha wananchi kiuchumi ndio maana inasogeza huduma zikiwamo za kifedha jirani yenu. Kila mmoja aangalie fursa zilizopo kukuza uchumi wake,” amesisitiza Rais huyo.

 

Alipozindua kampeni zake, Septemba 12 mwaka 2020 kwenye Uwanja wa Demokrasia uliopo Kibandamaiti Mjini Unguja, Dkt Mwinyi aliahidi mambo kadhaa atakayoyafanya endapo atachaguliwa kuiongoza SMZ ikiwamo kuimarisha uchumi wa bluu, kilimo na kuwawezesha wananchi kwa mitaji.

Kati ya pikipiki 272 zilizokabidhiwa Jana, 222 zilitolewa kwa vijana wa Mkoa wa Pemba Kaskazini na 50 kwa Pemba Kusini huku mkoa ukipata nusu ya boti 94 zilizokuwapo ambazo 32 ni kwa ajili ya kilimo cha mwani, na 15 kwa ajili ya uvuvi.

 

Vilevile, Rais alikabidhi hundi za mkopo kwa vikundi vitatu zenye thamani ya Sh273.8 milioni. Mikopo hiyo ilitolewa kwa Chama cha Ushirika Shirikani (Sh210.8 milioni), Chama cha Ushirika Umoja ni Nguvu (Sh58.8 milioni) na Chama cha Ushirika Mategemeo kilichopokea Sh5 milioni.

 

Mapema Februari, SMZ iliingia makubaliano na Benki ya CRDB kuwakopesha wananchi bila riba ikiikabidhi benki hiyo Sh60 bilioni zitakazokuwa zikitolewa kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kuanzia Januari mpaka Juni, wamekopesha Sh23.5 bilioni kwenye matawi matatu yaliyokuwapo na anaamini wananchi wa Wete sasa wanayo fursa ya kulitumia tawi hilo linalofanya jumla kuwa manne visiwani hapa.

 

“Wananchi wanaweza kupata huduma zetu pia kupitia makala 280, tulionao Unguja na Pemba. Mheshimiwa Rais ulitupa changamoto ya kusogeza huduma kwa wananchi na leo tumefika Wete,” amesema Nsekela.

 

Mkurugenzi huyo alisema wataendelea kushirikiana na Serikali kufanikisha miradi ya maendeleo ukiwamo utekelezaji wa program ya inuka na uchumi wa buluu inayolenga kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa zilizopo baharini.

 

Kwenye Sh60 bilioni zilizotolewa na Serikali, Nsekela alisema tayari jumla ya Sh6.7 bilioni zimekopeshwa kwa vikundi 607 vikiwamo 58 vya wilayani Wete. Vikundi hivyo vyote, vina wanachama 11,806 wakijumuisha 689 wa Wete waliopokea Sh529.6 milioni.

 

Akizungumzia umuhimu wa sekta binafsi katika kujenga uchumi, Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ, Dkt Saada Mkuya alisema taasisi za fedha zinachangia asilimia 3.4 kwenye pato la Taifa kwa mwaka.

 

Leave A Reply