RAIS wa Urusi, Vladimir Putin, ameamuru watu wa nchi hiyo kutokwenda kazini na kusalia majumbani hadi mwishoni mwa mwezi huu Aprili kama sehemu ya juhudi za kuzuia kusambaa kwa virusi hatari vya corona na pia watalipwa mishahara yao.
Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni, amesema anarefusha muda wa kutofanya kazi kwa muda wa wiki tatu zaidi na kwamba baadhi ya viwanda vinavyozalisha bidhaa muhimu vitaendelea kufanya kazi na maduka ya vyakula na dawa yanaruhusiwa kufunguliwa.
Ameongeza kamba mkakati wa Urusi wa kudhibiti kusambaa kwa corona umefanikiwa lakini ameonya kuwa idadi ya watu walio na maambukizi ya virusi hivyo itaendelea kuongezeka ambapo hadi kufikia sasa Urusi ina visa 4149 na vifo vya watu 34 huku waliopona wakiwa ni 281.
Covid-19 inaendelea kuathiri nchi mbalimbali duniani, huku maambukizi yake duniani yakifikia milioni 1.021, na watu wakiendelea kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
Marekani inaendelea kuripoti visa vingi vya maambukizi ya virusi vya Corona, ambapo vifo vya watu 1,169 vimeripotiwa ndani ya saa 24 zilizopita.
Leo Ijumaa, hadi habari hii inachapishwa, watu 25 wamefariki kwa ugonjwa huo nchini Marekani ambapo 132 wamefariki nchini Ubelgiji.