The House of Favourite Newspapers

Rais Ruto aapa kukabiliana na waandamanaji wanaopinga mswaada wa fedha – Video

Rais wa Kenya, William Ruto, katika hotuba kwa taifa Jumanne, amesema kuwa matukio ya vurugu yaliyoshuhudiwa Jumanne ambapo waaandamanaji walivunja uawla bunge na kuingia ndani na kusababisha uharibifu mkubwa, ni kitendo cha uhaini.

“Cha kusikitisha zaidi ni kwamba mashambulizi ya leo (Jumanne) dhidi ya utaratibu wa kikatiba wa Kenya yamesababisha watu kupoteza maisha, uharibifu wa mali na kuzibeza taasisi na nembo za mamlaka yetu,” Ruto anasema.

Ruto ameongeza kuwa serikali yake itatimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuwalinda raia wa Kenya dhidi ya kila aina ya madhara, na kuwaonya wale alioataja ni “wapangaji, wafadhili, waandaaji na watetezi wa ghasia na machafuko” yaliyoshudiwa Jumanne jijini Nairobi na miji mingine ya nchi hiyo.

“Si jambo la haki na kistaarabu kufikiriwa kwamba wahalifu wanaojifanya waandamanaji wa amani wanaweza kusababisha ugaidi na vurugu dhidi ya wananchi, wawakilishi wao waliowachagua na taasisi zilizoanzishwa chini ya katiba yetu na kutarajia kuachiliwa huru,” rais Ruto amekariri.

Ruto anadai kuwa maandamano hayo yalitekwa nyara na wahalifu hatari ambao wamelisababishia taifa hasara na hivyo ameviagiza “vyombo vyote vya usalama vya taifa kuchukua hatua zote za kuzuia majaribio yoyote ya wahalifu hatari ya kuhujumu usalama na utulivu wa nchi yetu.”

“Nalihakikishia taifa, kwamba Serikali imekusanya rasilimali zote kwa ajili ya taifa ili kuhakikisha kwamba hali ya aina hii, haitajirudia tena, kwa gharama yoyote ile.”

Hata hivyo, Ruto hajaeleza iwapo ataridhia malalamiko ya wananchi kwa kufanyia marekebisho ya mswaada wa fedha uliozua utata.