Rais Ruto Alivyowasili Dar kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt. William Ruto leo Januari 28, 2025 ameongeza idadi ya Marais wa Afrika waliowasili jijini Dar es Salaam kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati na kufikia 20. Rais Ruto ameungana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unaoendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Zanzibar, Mheshimiwa Shaabani Ali Othman, alimkaribisha Mheshimiwa Rais Ruto alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na Marais, mkutano huu unahudhuriwa pia na Makamu wa MaRais, Mawaziri Wakuu, Manaibu Mawaziri Wakuu, na mawaziri wengine wanaowakilisha Wakuu wa Nchi zao.
Mawaziri wa Fedha na Nishati kutoka nchi za Afrika pia wanahudhuria mkutano huo.
Mkutano huo ulianza tarehe 27 Januari,2025 kwa majadiliano ya ngazi ya mawaziri, na tarehe 28 Januari 2025, Wakuu wa Nchi wanakutana ili kuhitimisha mkutano huo.
Mkutano huo unatarajiwa kupitisha Azimio la Dar es Salaam, ambalo linasisitiza dhamira ya pamoja ya viongozi wa Afrika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu barani Afrika ili kuunga mkono maendeleo ya bara hili.