The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Aagiza Milioni 960 za Uhuru Zijenge Mabweni Katika Shule nane za Msingi

0
Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza TZS milioni 960 ambazo zilitengwa katika bajeti kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe za Uhuru inayoadhimishwa kila Desemba 9, zipelekwe Ofisi ya Rais TAMISEMI na zitumike kujenga mabweni katika shule nane za msingi zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 5, 2022 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu, George Simbachawene amezitaja shule hizo kuwa ni Buhangija (Shinyanga), Goeko (Tabora), Darajani (Singida), Mtanga (Lindi), Songambele (Manyara), Msanzi (Rukwa), Idofi (Njombe), na Longido (Arusha).

Amesema shule hizo zimekwisha ratibiwa na TAMISEMI na tayari zimekwisha gawiwa fedha hizo kwa ajili ya kuwajengea mazingira rafiki wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

“Ikiwa ni dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwajali na kuwajengea mazingira rafiki watu wenye mahitaji maalum hapa nchini, hili ni jambo kubwa na la kishujaa na la kupongezwa sana,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kwa wingi katika midahalo na makongamano katika wilaya zote na kujadili kwa kina kuhusu maendeleo endelevu katika siku ya maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania.

ZUCHU HAWEZI KUJIBISHANA na MA-X WA DIAMOND, SIRI YAFICHUKA WEMA KUBEBA UJAUZITO | HOTPOT

Leave A Reply