The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Aanza Ziara Mkoani Arusha, Apokelewa Na Magari Ya Utalii Zaidi Ya 500 (Picha +Video)

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi wa dini, wadau wa utalii pamoja na wageni mbalimbali waliofika kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) tarehe 27 Novemba, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapongeza wakazi wa Mkoa wa Arusha wakiwemo Viongozi wa dini na wadau wa Utalii kwa kuendelea kutunza Amani na utulivu, suala ambalo limechangia Ongezeko kubwa la idadi ya watalii pamoja na mikutano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi hizo Jumatano Novemba 27, 2024 alipokuwa akizungumza na Wakazi wa Mkoa wa Arusha, waliofika kumlaki kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro KIA, Akielekea Mkoani Arusha kwenye ziara ya Kikazi ya siku nne.

Viongozi wa dini, wadau wa utalii pamoja na wageni kutoka maeneo mbalimbali wakiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 27 Novemba, 2024

Akiwashukuru Mamia ya Wafanyabiashara na wadau wa utalii waliofika kumpokea na magari ya kitalii zaidi ya 500, Rais Samia amesema suala hilo limekuwa la heshima kubwa kwake na linampa moyo na ari zaidi ya kuwatumikia watanzania, akiahidi kurudi Mkoani Arusha kwaajili ya kuzungumza na wafanyabiashara na wadau hao wa utalii.

Akimkaribisha Mkoani Arusha, Mkuu wa Mkoa huo Paul Christian Makonda  amesema hatua ya Rais Samia kuruhusu Chanjo ya Corona kuingia nchini Tanzania Julai 2021 pamoja na kushiriki kwenye Filamu ya Royal Tour mwaka 2022, kumekuwa na faida kubwa kwa uchumi na utalii wa Mkoa wa Arusha suala ambalo limeathiri Pato la Mkoa wa Arusha na Uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

Rais Samia akiwa katika picha ya pamoja na watoto wakati wa mapokezi yake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Mkoani Arusha leo Alhamisi anatarajiwa kutunuku Kamisheni kwa Maafisa wanafunzi katika chuo cha mafunzo ya Kijeshi Monduli, kushiriki kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki pamoja na kuwa na mkutano na Viongozi wa jamii ya Kimasai mkoani Arusha.

Rais Dkt. Samia akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Leave A Reply