The House of Favourite Newspapers

Rais Samia agoma ombi la wananchi kumwondoa mwekezaji

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Kilwa Masoko Mkoani Lindi ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika Mikoa ya Kusini tarehe 19 Septemba, 2023.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amekataa ombi la wananchi lililotaka afute hati ya umiliki ardhi inayodaiwa kuporwa kinyume cha sheria na mwekezaji Kampuni ya Kilwa Yark Club na kuwataka waridhie uwekezaji huo kwa kuwa una lengo la kuleta maendeleo.

Uamuzi huo wa Rais Samia umetolewa Septemba 19, 2023, baada ya Mbunge wa Kilwa Kusini, Ally Kisinge, kumuomba afute hati hiyo ili eneo hilo la kiwanja namba 106 lililoko karibu na Pwani ya Jimbiza, lirudi kwa wananchi kwa ajili ya kutekeleza shughuli za uvuvi.

“Kama hili eneo liko chini ya kilomita moja kutoka bandari sasa hao wavuvi unaowatetea pale ni wapi? Sababu kwenye bandari kuna eneo la wavuvi wadogo na ndiyo hapa watakapoleta mazao yao. Sijui mnataka tufute eneo hili ili mpate kitu gani? Watu wa Kilwa badili ya kurudi nyumba naomba tuwe na mawazo ya kwenda mbele,” amesema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi amesema “mbunge unaweza kusema haya kuwafurahisha watu wake lakini mantiki ya hili ni nini? Ningefurahi ungesema kama kashindwa alirudishe tutafute mwekezaji mwingine na sio tufute hati wavuvi warudi kule halafu iwe nini? Maendeleo makubwa yapo hapa badala ya kwenda mbele tunarudi nyuma hebu tujiangalie vizuri.”

Aidha, Rais Samia alisema akilitekeleza mgogoro wa kiuwekezaji utaibuka na hatimaye Serikali kutakiwa kulipa fedha nyingi kwa ajili ya fidia.

“Ndugu zangu huu ni mgogoro na mwekezaji, kama mwekezaji alishapewa ardhi na hajasema kashindwa kutekeleza eneo lile, mnaposema Serikali ikafute hati tunapelekwa mahakamani na Serikali tunakwenda kulipa fedha nyingi sana,” amesema Rais Samia.

Kabla ya Kasinge kuwasilisha ombi hilo kwa Rais Samia, mnamo Julai mwaka huu, baadhi ya wafanyabiashara katika Bandari Kavu ya Jimbiza, kupitia mtandao huu waliiangukia Serikali yake wakitaka wasiondolewe katika eneo hilo wakikataa kumpisha mwekezaji huo.

Walidai Kampuni ya Yark Club ilipewa ardhi kinyume cha sheria, huku wakidai sehemu ya eneo hilo liko kisheria kwa ajili ya shughuli za kijamii , kwani liko ndani ya mita 60 kutoka ufukwe wa bahari.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai alikanusha madai hayo akisema mwekezaji analimiliki kihalali.

Leave A Reply