
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema alishtushwa na taarifa za wachezaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) kudai kugoma kusafiri kwenda Morocco kabla ya Fainali za AFCON 2025, wakilalamikia posho zao.
Akizungumza Januari 10, 2026 katika hafla ya kuipongeza Taifa Stars kwa mafanikio yao, Rais Samia amesema taarifa hizo hakuzipokea kwa namna nzuri, hata hivyo alifarijika kuona kuwa mgomo huo haukufanyika.

“Jicho letu liwe kwa vijana wetu. Kuwafanyisha mazoezi ni muhimu, lakini pia kuzingatia maslahi yao. Kuna siku nilikuwa nimekaa, mara paap napokea taarifa kutoka vyombo vyangu vya serikali kwamba wachezaji wamegoma kwenda Morocco kutoka Misri.
“Nikasema nini? Kiposho kidogo hakitoshi? Mungu wangu wee! Nikamwita Makonda (Paul) nikamuuliza haya mnafanyaje kuhusu hili? Sitaki vijana wetu wawe wameshuka morali kwa namna yoyote, ebu changamka basi,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameongeza kuwa alifurahishwa na hatua ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alipotangaza dau la shilingi milioni 200 kwa timu hiyo, hatua aliyosema ilisaidia kurejesha morali ya wachezaji.
“Mara paap namsikia Makonda anatangaza dau la milioni 200, nikasema yes, hivyohivyo,” ameongeza.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa serikali itaendelea kujitahidi kuhakikisha wachezaji wa Taifa Stars wanapata stahiki zao kwa wakati ili kuwawezesha kuwakilisha taifa kwa morali na ari ya juu.



