The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Aomboleza Kifo cha Mkurugenzi wa TANESCO na Dereva Wake

Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, Tanesco.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya Mhandisi Boniface Gissima Nyamohanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), pamoja na dereva wake, Muhajiri Mohammed Haule, vilivyotokea usiku wa kuamkia leo kwa ajali ya barabarani eneo la Bunda, Mkoa wa Mara.

“Ninatoa pole kwa familia, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, watumishi wa TANESCO, ndugu jamaa na marafiki.

“Namuomba Mwenyezi Mungu azijaalie familia, ndugu, jamaa na marafiki subra, uvumilivu na moyo wa ibada katika kipindi hiki kigumu.

“Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi,” aliandika Rais Samia kwenye akaunti zake rasmi za mitandao ya kijamii.