The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Kuongoza Mazishi ya Hayati Edward Lowassa Monduli, Arusha… Ratiba Ipo Hapa -Video

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa na Mkewe Mary Majiwa, akisaini kitabu cha maombolezo, kwenye msiba wa aliyekua Waziri Mkuu Mstaafu, Marehemu Edward Lowassa, nyumbani kwake Masaki, jijini Dar es Salaam, Februari 11.2024.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza Mazishi ya Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Lowassa yanayotarajiwa kufanyika Wilayani Monduli Mkoani Arusha Jumamosi Februari17, 2024.

Awali Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kuanzia tarehe 10 Februari, 2024.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akiongea na Mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, Mbunge wa Jimbo la Monduli, Fred Lowassa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo Jumapilii, Februari 11, 2024 wakati akitoa taarifa ya ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo, Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Oysterbay, Dar es Salaam.

Amesema katika kipindi cha siku tano za maombolezo, Taifa litaendelea na shughuli za umma na kijamii sambamba na kushirikiana na wanafamilia katika ratiba ya msiba kama ilivyoandaliwa na kamati ya mazishi ya Kitaifa na wanafamilia.

Amesema kabla ya mazishi hayo mwili wa Hayati Lowassa unatarajiwa kuagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Amesema Jumanne Februari 13, 2024 mwili wa Hayati Lowasa unatarajiwa kuangwa na viongozi na wananchi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema Jumatano Februari 14 mwili wa Hayari Lowasa utapelekwa katika Kanisa la KKKT Azania Front kwa ajili ya ibada takatifu na kuaga.

Amesema Alhamisi Februari 15 mwili wa Hayati Lowassa utasafirishwa hadi jijini Arusha ambapo viongozi na wananchi watapa fursa ya kuaga katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid.

Waziri Mkuu huyo mstaafu alifariki jana (Jumamosi, Februari 10, 2024) wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam na tangazo la kifo chake lilitolewa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango

Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Edward Lowassa enzi za uhai wake.