The House of Favourite Newspapers

Rais wa Brazil ataka wanaocheza nje wazuiliwe

Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva amependekeza na kushauri Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini humo kuacha kujumuisha katika kikosi cha Timu ya Taifa wachezaji wanaocheza soka nje ya Brazil akidai kwamba wachezaji hao wa sasa hawana ubora kama waliokuwa nao nyota kama Garrincha na Romario.

 

Timu ya Taifa ya Brazil kwa sasa iko katika harakati za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2026 itakayofanyika katika nchi za USA, Mexico na Canada ambapo imekuwa na matokeo ya kusua baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Paraguay Septemba 11 mwaka huu na juzi ijumaa kupata ushindi wa tabu wa goli 2-1 dhidi ya Chile licha ya kikosi hicho kilichopo chini ya kocha Dorival Junior kuwa na mastaa kibao kama Vini, Rodrygo, Endrick, Allison, Ederson Moraes, Raphinha na nyota wengine wengi wanaocheza katika vilabu vikubwa barani Ulaya.

 

“Hao walioko nje sio wazuri kuliko hawa (wanaocheza ndani Brazil), Brazil kuna wachezaji wenye ubora kama wao (wanaocheza nje), hivyo toeni nafasi kwa hawa wanaocheza hapa”

Alisema Rais huyo ambaye anaamini kwa sasa hakuna wachezaji kama Romario au Garrincha waliokuwepo hapo nyuma, hata hivyo Rais uyo anatarajiwa kufanya kikao na rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini humo CBF, kwaajili ya mazungumzo zaidi.

Ikumbukwe, mapema Juni mwaka huu, alie wahi kuwa nyota wa Timu hio, Ronaldinho Gaucho alinukuliwa akikikosoa kikosi cha Timu ya Taifa ya Brazil na kusema kwamba hakina viongozi wanaoheshimika bali wachezaji wa kawaida wasio na mapenzi ya dhati na uchungu dhidi ya jezi ya timu hiyo.

 

Hata hivyo, Septemba 10, 2024 kocha Dorival katika mkutano na waandishi wa habari aliwatoa hofu wananchi na mashabiki wa Brazil kwa kuwaahidi kuwa Brazil itacheza mechi ya fainali ya michuano hio. Brazil itacheza mchezo wake mwingine wa kuwania kufuzu fainali hizo jumatano majira ya saa 9:45 usiku watakapowakaribisha Timu ya Taifa ya Peru.