The House of Favourite Newspapers

Rais wa Marekani Ashangazwa na Urusi Kusitisha Mkataba wa Nyuklia

Rais wa Marekani Joe Biden.

Rais wa Marekani Joe Biden ameutaja uamuzi wa Urusi wa kusitisha mkataba wa silaha za nyuklia wa New Start kuwa ni kosa kubwa.

Rais Vladimir Putin alitangaza hatua hiyo siku ya Jumanne katika hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa.

Mkataba huo uliowekwa saini mwaka 2010, unaweka kikomo katika idadi ya silaha za nyuklia za Marekani na Urusi na kila nchi ina uwezo wa kukagua silaha za mwenzake.

Bw Biden alitoa maoni yake juu ya hilo alipokutana na kundi muhimu la washirika wa Nato nchini Poland.

Kundi la mataifa ya mashariki mwa Ulaya, linalojulikana kama Bucharest Nine, lilinukuliwa kulaani kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine karibu mwaka mmoja tangu kuanza kwake.

Uamuzi wa Putin wa kusitisha kuhusika katika mkataba wa nyuklia yalipitishwa na mabunge yote mawili ya Urusi siku ya Jumatano.

Lakini wizara ya mambo ya nje ya Urusi baadaye ilisema Urusi itaendelea kuzingatia vikwazo vya mkataba wa New Start katika “mbinu ya kuwajibika”.

Afisa mkuu wa kijeshi aliliambia bunge dogo la Urusi kwamba nchi hiyo itaendelea kuzingatia vikwazo vilivyokubaliwa katika mifumo ya utoaji wa nyuklia ikimaanisha makombora na ndege za kimkakati za kushambulia.