The House of Favourite Newspapers
gunners X

Rais wa Ufaransa Aomba Msaada Kulijenga Upya ‘Notre Dame’

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

RAIS  wa Ufaransa ameahidi kupata misaada ya kimataifa katika kulijenga upya kanisa kongwe la Notre Dame jijini Paris baada ya sehemu ya kanisa hilo kuteketea kwa moto na kuharibika.

Maofisa wa zima-moto walifanikiwa kuliokoa jengo hilo la kihistoria lenye miaka 850 lakini paa na mnara wa jengo hilo vimeanguka.

Moto huo ulidhibitiwa saa tisa baadaye baada ya kuanza.  Chanzo chake hakijajulikana lakini maofisa wamesema huenda kikahusishwa na ukarabati mkubwa unaoendelea.

Ofisi ya mwendesha mashtaka imesema inachunguza mkasa huo, na kwamba  ofisa mmoja wa zima-moto alijeruhiwa kiasi wakati akikabiliana na moto huo, kamanda Jean-Claude Gallet ameiambia televisheni ya BFM.

Moto huo ulizuka  mnamo saa kumi na mbili na nusu kwa saa za Ufaransa na kulikumba jengo hilo  ambalo ni moja ya makanisa maarufu na linalotembelewa na idadi kubwa ya watalii kutoka pande mbalimbali duniani kila mwaka.

Sehemu kubwa ya paa la jengo la kanisa hilo imeteketezwa na moto ambapo mwingine ukifanikiwa kuzimwa kabla ya kufika  katika minara miwili ya kengele.

Hadi tunakwenda mitamboni, wazimamoto wanafanya kila juhudi kuokoa vito vya thamani vilivyomo ndani ya kanisa hilo na pia kuzuia mnara wa upande wa kaskazini kuporomoka.

Maelfu ya watu wamekusanyika katika barabara zilizo karibu na kanisa hilo kushuhudia mkasa huo wakiwa kimya.

Baadhi yao walionekana wakidondokwa na machozi, huku wengine wakiimba nyimbo za sifa na kumwomba Mungu.

Makanisa kadhaa nchini Ufaransa yamekuwa yakipiga kengele kuashiria uharibifu wa moto huo.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambaye alifika katika eneo la tukio, amesema mawazo yake yako na “waumini wote wa Kanisa Katoliki na Wafaransa wote kwa jumla.  Kama na watu wengine nchini, nimesikitika sana kuona sehemu ya maisha yetu ya kila siku ikiteketea.”

 

CHANZO: BBC SWAHILI

 

Comments are closed.