Rais wa Zamani wa Angola, Eduardo dos Santos Afariki Dunia
Rais wa Zamani wa Angola, Eduardo dos Santos akiwa kwenye moja ya mikutano aliyowahi kuhudhuria enzi ya uhai wake
RAIS wa zamani wa nchi ya Angola Eduardo dos Santos amefariki dunia siku ya Ijumaa ambapo ofisi ya Rais nchini Angola imethibitisha taarifa hizo.
Rais Eduardo dos Santos aliitawala Angola kwa takribani miongo minne na hivyo kuingia kwenye orodha ya viongozi wa Afrika ambao wamewahi kukaa madarakani kwa muda mrefu zaidi ambapo aliachia madaraka miaka mitano iliyopita na kukabidhi uongozi kwa Joao Lourenco ambaye ni Rais wa sasa wa Angola.
Kiongozi huyo wa zamani aliyekua na umri wa miaka 79, alifariki katika zahanati ya Teknon mjini Barcelona, Uhispania ambako alikua anapata matibabu kufuatia ugonjwa wa muda mrefu.
Itakumbukwa kwamba utawala wake uligubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu karibu miaka 30 dhidi ya waasi wa kundi la UNITA lililokua linaungwa mkono na taifa la Marekani.
Rais wa sasa wa Angola Mhe. Joao Lourenco, ametangaza siku 5 za maombolezi ya kitaifa na kumuelezea dos Santos kama “mtu wa kipekee nchini Angola.”
Licha ya kwamba alichaguliwa na dos Santos mwenyewe kuchukua nafasi yake, Lourenco mara moja alianza uchunguzi kuhusu tuhuma za ulaji rushwa wa mabilioni ya dola zilizokuwa zikimuhusu mtangulizi wake Hayati Eduardo dos Santos.
Viongozi mbalimbali na duniani kote wameanza kutoa salamu zao za rambirambi kwa serikali ya Angola ikiwemo Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye amemuelezea kiongozi huyo kuwa amesaidia katika vita vyao dhidi ya utawala wa wazungu na hatimaye kupelekea uhuru wan chi hiyo.