Kartra

Rasmi Gadiel, Ajibu Wafyekwa Simba

RASMI uongozi wa Simba umetangaza kuachana na wachezaji wake wawili kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajibu na beki wa kushoto Gadiel Michael.

 

Simba inaachana na wachezaji hao kama wachezaji huru kutokana na mikataba yao kutarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

 

Awali tetesi zilizagaa za wachezaji hao kuwepo katika mipango ya kusajiliwa na Yanga katika kuelekea msimu ujao kabla ya mashabiki kuja juu kushinikiza viongozi kusitisha mipango hiyo.

 

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Simba, timu hiyo haipo tena katika mipango ya kuwaongezea mikataba mipya ya kuendelea kuichezea timu hiyo, ni baada ya Benchi la Ufundi kupendekeza kuachana na nyota hao.

 

Chanzo hicho kilisema kuwa Simba tayari imempata mbadala wa Gadiel ambaye ni Edward Charles Manyama aliyesaini mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kumpa changamoto ya ushindani wa namba, Mohammed Hussein Zimbwe.

 

Kiliongeza kuwa mabosi hao hivi sasa wapo katika mipango ya kumpata kiungo mwingine mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao atakayemrithi Ajibu.

 

“Rasmi Gadiel na Ajibu ruksa hivi sasa kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayowahitaji katika kuelekea msimu ujao, kwani hawapo katika mipango yetu.

 

Hivi sasa ni wachezaji huru kwani mikataba yao tayari imemalizika, kwani wale wachezaji wetu wote muhimu waliokuwepo kwenye mipango ya kocha tumewaongezea mikataba mipya baadhi ni Kakolanya (Beno), Bocco (John), Kapombe (Shomari), Nyoni (Erasto), Mkude (Jonas) na Kagere (Meddie).”

 

Akizungumzia usajili wa timu hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, alisema: “Muda wa usajili bado, lakini pia mipango yote ya usajili ipo kwa kocha wetu Gomes (Didier) ambaye ndiye atakayependekeza wachezaji wa kusajiliwa na kuachwa.”

 


Toa comment