Rasmi TFF Yatangaza Kuipoka Simba Pointi 3, Yazirudisha Kwa Kagera Sugar
Mambo yamezidi kuwa mambo katika soka la Tanzania hiyo ni baada ya Shirikisho la Soka la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutangaza kufuta maamuzi ya kuipa Simba pointi tatu katika mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar.
Simba ilipoteza mchezo dhidi ya Kagera kwa kufungwa mabao 2-1, wiki mbilizilizopita katika Uwanja wa Kaitaba, Kagera katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara lakini baadaye ilikata rufaa ikipinga Kagera kumtumia mchezaji Mohamed Fakhi ikidai alikuwa na kadi tatu za njano, ndipo ikapewa ushindi huo kupitia Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji Ligi Tanzania maarufu kwa jina la Kamati ya Saa 72.
Mara baada ya kamati hiyo kuipa Simba pointi Kagera ikaomba kupitiwa upya kwa suala hilo na ndipo TFF ikatangaza kuwa suala hilo sasa litakuwa chini ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ambayo ndiyo imetoa maamuzi hayo.
Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amezungumza nawaandishi wa habari na kufafanua juu ya suala hilo ambapo amesema kuna sababu kadhaa zimechangia kuchukuliwa kwa maamuzi hayo ambapo alisitaja kuwa ni:
“Malalamiko ya Simba hayakuwasilishwa kwa wakati muafaka tangu mchezo ulipochezwa, malalamiko yao hayakuwa katika njia ya maandishi, rufaa ya Simba haikulipiwa ada, kikao cha Kamati ya Saa 72 kilikosa uhalali kutokana na kuwashirikisha watu ambao hawana uhalali wa kuwa kwenye kikao.
“Kutokana na sababu hizo kamati imeamua kufuta maamuzi yaliyochukuliwa na Kamati ya Saa 72 na kurejesha matokeo kama yalivyokuwa, pia kamati imemuagiza katibu mkuu wa TFF kuwapeweleka baadhi ya wajumbe wa bodi ya ligi katika Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kwenda kinyume na kazi zao,” alisema Mwesigwa.