The House of Favourite Newspapers

RAY C, ACHA KUKATISHA TAMAA WENZAKO, PAMBANA NA HALI YAKO!

Mwanadada Rehema Chalamila ‘Ray C’.

HABARI zinazotingisha kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa, ni kuhusu bifu jipya kati ya mwanadada Rehema Chalamila ‘Ray C’ na mwanamitindo ambaye pia ni mzazi mwenzake Diamond Platnumz, Hamisa Mobeto.

Kwa wasiojua kinachoendelea, kuna vita kati ya wanadada hawa wawili, Ray C analeta ‘chokochoko’ kwa Hamisa na kama ujuavyo, Hamisa naye anamiliki ‘jeshi’ la mtandaoni, ambalo kazi yake ni kuwatusi wote wanaoonekana kuwa maadui wa bosi wao huyo, kwa hiyo mambo ni moto kwelikweli.

Mwanamitindo ambaye pia ni mzazi mwenzake Diamond Platnumz, Hamisa Mobeto.

Chanzo cha yote, ni baada ya mwanadada Hamisa Mobeto ambaye kwa kipindi kirefu amekuwa akijishughulisha na masuala ya u-video queen na mitindo, kutoa wimbo uitwao Madam Hero! Kwa kifupi Hamisa naye ameamua kuingia kwenye muziki wa kizazi

Kipya, Bongo Fleva na tayari ana wimbo mmoja aliouachia siku chache zilizopita.

Sasa baada ya mwanadada huyo kujiongeza kwenye muziki, Ray C kwa kutumia akaunti yake ya Instagram, akatokwa povu kwelikweli. Katika akaunti yake, aliandika: Mnaharibu maana nzima ya Bongo Fleva, acheni utani na kazi za watu, siyo lazima kila mtu aimbe, it’s (akaweka tusi).

Japokuwa hakumtaja mtu yeyote jina, lakini ilionesha dhahiri kwamba mlengwa ni Hamisa Mobeto kwa sababu ujumbe huo ulikuja muda mfupi baada ya mwanadada huyo kuachia ngoma yake ya Madam Hero.

Team Mobeto wakaja juu na kuanza kumvurumishia mitusi Ray C ambaye naye baadaye uzalendo ulimshinda, akaja na povu jingine na safari hii ikaonesha dhahiri kwamba kumbe ni kweli dongo lake la awali alimlenga Hamisa.

Kwa wafuatiliaji wa mambo, watakumbuka kwamba hii si mara ya kwanza kwa Ray C kum-attack Mobeto. Miezi michache iliyopita, aliwahi pia kumshambulia mwanadada huyo akidai kwamba anauza nguo feki zenye lebo ya Fendi kwa bei kubwa kwenye duka lake, wakati nguo hizohizo zinapatikana Kariakoo kwa bei chee.

Mengi yalizungumzwa lakini ukweli unabakia kuwa Ray C aliharibu ‘brand’ ya mwenzake kwa makusudi na sijui hili lilimuathiri Mobeto kwa kiasi gani, kwa sababu alikuwa ameilenga biashara yake ya duka la nguo moja kwa moja.

Hii si mara ya kwanza kwa Ray C kuwatolea mapovu ‘wadogo zake’ mitandaoni. Siku za nyuma, aliwahi kumshukia vikali mwanadada Nandy kwa madai kwamba alikuwa akiimba ‘cover’ ya nyimbo za Ray C kwenye shoo zake bila ridhaa yake.

Akaenda mbali na kutoa tuhuma nyingine kadhaa kwa Nandy na wenzake lakini kwa bahati nzuri, binti huyo mdogo alimjibu kwa busara sana na suala hilo likayeyuka.

Unajaribu kujiuliza, kwa nini Ray C, ambaye kila mmoja anamfahamu kama miongoni mwa wanadada walioupigania muziki wa kizazi kipya na kuupa heshima, anakuwa na roho ‘nyeusi’ kiasi hiki?

Tukianza kwa suala la Mobeto, ni mwanamke mwenzake, tena mdogo wake ambaye anajitahidi kupambana kwa kutumia njia halali kuhakikisha anajikwamua kiuchumi. Alianza na uvideo queen, mitindo, ujasiriamali na sasa ameingia kwenye muziki, kwa nini Ray C anamkatisha tamaa badala ya kumpa sapoti?

Kuisema vibaya biashara ya mwenzako unamaanisha akose wateja, mtaji uyumbe na mwisho afunge biashara yenyewe kwa kushindwa kulipa kodi kutokana na kukosa wateja, Ray C unataka Hamisa aje kuishi maisha ya aina gani?

Kwenye ishu ya Nandy, hutaki mwenzako japo aimbe ‘cover’ ya nyimbo zako, tena kwa heshima kama ishara ya kukuenzi na kukukubali, ina maana Ray C umesahau kwamba hata wewe uliimba baadhi ya nyimbo za wakongwe waliokutangulia na zikakupa umaarufu?

Acha kuwawekea wenzako mtima nyongo, kila zama zina kitabu chake! Huu ni wakati wa hawa vijana kuonesha kile Mungu alichowajaalia, acha kuwawekea mtima nyongo usio na maana, isitoshe ushakuwa mtu mzima sasa unapaswa kuwa mfano wa kuigwa, period!

NA HASH POWER

Hamisa Mobetto – Madam Hero (Official Audio)

Comments are closed.