Ray C Afichua Siri Yake na Kanumba

MSANII mkongwe wa filamu Bongo, Vincent Kigosi ‘Ray’ kwa mara ya kwanza amefichua siri inayomhusu yeye na msanii mwenzake marehemu Steven Charles Kanumba.
Hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Ray kuposti picha yake akiwa na marehemu Kanumba katika mtandao wake wa Instagram, kisha kukumbushia jinsi walivyokuwa wakiishi hapo zamani.
Alivyoposti hivyo, aliibuka shabiki mmoja na kumwambia kuwa ni mnafiki na hampendi kweli Kanumba kama anavyojionyesha kwa watu.
Baada ya kuambiwa hivyo, Ray naye hakutaka kulaza damu, alimjibu shabiki huyo palepale hivyo kusababisha ishu hiyo kuwa gumzo mitandaoni na ndipo RISASI likamtafuta Ray:
Risasi: Naona umechafua hali ya hewa uko mtandaoni, kunani tena?
Ray: Unajua watu wengi wamemjua Kanumba baada ya kufa na asilimia kubwa watu wa Instagram hawamjui vizuri, kwa hiyo ni watu ambao wanaenda na upepo tu, wakiona huyu kamposti kasema hiki, basi na wao wanaelewa hivyo hivyo.
Ndio maana wanasema kwamba eti Kanumba amekufa na Ray amekufa, kwa maana ya kwamba mimi nilikuwa nabebwa na Kanumba wakati hawajui kama mimi ndio nilimtoa Kanumba.
Ndio maana nasema kuna vitu vingine hupaswi kuzungumza na watu kwa sababu ni wajinga hawaelewi.
Mimi nilianza kuwa muigizaji maarufu kabla ya Kanumba, nilianza kucheza filamu na kina Aunt Ezekiel nikiwa tayari najulikana, kuna Tamthiliya moja tulicheza ilikuwa inaitwa Sayari au Taswira kama sikosei, kipindi hicho nina jina kubwa wakati Kanumba akiwa hajulikani, Johari, Mainda, Thea; wote hawajulikani.
AMWAGA SIRI…
Baada ya hapo, Kanumba alikuwa anasoma Jitegemee, akawa anakuja amevaa kaoshi nyekundu anakaa nje ya Kaole, siku zilivyozidi kwenda, Kanumba akaja kutunga stori ya Johari, kiongozi wetu ndio akanichagua mimi niisimamie kwa sababu mimi ndiye nilikuwa mkubwa kwa kipindi hicho.
Mwisho wa siku tukachangiana ‘idea’ hadi tukaicheza, hapo ndipo Kanumba alipoanza kujulikana.
Kitu kingine, watu wameanza kumuongelea sana Kanumba wakati amefariki, lakini kipindi yupo hai, walikuwa wanasema eti tunauza sura, mara tuache kuigiza waigize watu wengine.
Kuna kipindi Kanumba alienda Big Brother, wakamtukana kuwa hajui Kiingereza, leo hii amefariki ndipo wanammwagia sifa kibao, kwa hiyo baadhi ya Watanzania hawawezi kumpa mtu sifa zake angali yupo hai.
Sasa hivi watu wanaongea kuwa tangu kanumba amefariki, Ray hamna kitu, sio kweli wanaona hivyo kwa sababu hakuna tena ushindani, hata leo hii Yanga ikifa, Simba haitakuwepo. Hivyo tasnia yoyote kama haina mshindani, lazima itashuka kidogo.
Risasi: Kwa nini ishuke?
Ray: Kwa sababu hamasa inakuwa haipo, lakini nitawahakikishia kwenye hii Tamthiliya yangu inayokuja kuwa mimi ni msanii mkubwa na ni wa tofauti na wasanii wengine wote mnaowaona nyinyi.
STORI | Memorise Richard, RISASI

