RC Chalamila Apokea Melivita Ya Matibabu Ya Jeshi China Maarufu Kwa Jina la ‘Peace Ark’
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Julai 16,2024 amepokea Melivita ya matibabu iitwayo Peace Ark ya Jeshi la ukombozi la watu wa China katika Bandari ya Dar es Salaam.
RC Chalamila akiongea wakati wa mapokezi hayo amesema Melivita hiyo itakuwepo katika Mkoa wetu kutoa huduma za kitabibu kwa wakazi wa mkoa huu na watanzania kwa ujumla kuanzia tarehe l16 Julai, 2024 hadi tarehe 23 Julai,2024 ambapo leo Julai 16, 2024 ni siku maalum ya uzinduzi, na kuanzia tarehe 18-23 Julai 2024 ndyio siku rasmi ya kuanza kutoa matibabu kwa wananchi.
Huduma hizo za kitabibu zinatolewa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka sitini(60) ya ushirikiano kati ya Tanzania na China na maadhimisho ya miaka sitini (60) tangu kuanzishwa kwa JWTZ tarehe 01 Septemba,1964.
Aidha RC Chalamila amesema huduma za kitabibu zinazotarajiwa kutolewa ni pamoja na vipimo, tiba za kawaida pamoja na upasuaji wa kawaida, magonjwa ya kina mama, mifupa, njia ya mkojo, macho, pua, koo, meno, moyo, utumbo pamoja na ngozi zilizoungua na moto ambapo matibabu hayo yatatolewa kwa ushirikiano wa wataalamu wa Afya wa JWTZ, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Tumbi, Amana, Mwananyala, Temeke na Jeshi la China.
Vilevile kutakuwa na kikundi cha Madaktari Bingwa watakaokuwa wanakwenda kutoa matibabu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mbagala , Hospitali ya Lugalo na Kunduchi, Hospitali ya Amana, Bunju, Mwananyamala na Temeke pamoja na maeneo mengine ambayo ratiba rasmi itatolewa na JWTZ.
Sanjari na hilo amesema wananchi watakaokwenda Bandarini kwenye Meli hiyo kwa ajili ya kupata matibabu wanataarifiwa wapitie geti namba mbili(2) la Bandari ya Dar es salaam.
Mwisho RC Chalamila amesema Matibabu hayo yatatolewa bure, hivyo ametoa rai kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo kujitokeza kwa wingi kuitumia fursa hiyo ya kitabibu.