The House of Favourite Newspapers

RC Makalla Ahimiza Ushirikiano Katika Kuwaletea Maendeleo wananchi

0

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makalla ametoa rai kwa Viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kushirikiana naye kwa dhati ili kutoa huduma bora na kuwaletea maendeleo wananchi.

Mhe. Makalla amesema hayo mapema leo Mei 31, 2023 wilayani Nyamagana wakati akizungumza na Viongozi, watendaji na Makundi mbalimbali yakiwemo ya wanasiasa, wafanyabiashara na kamati ya Amani ya Wilaya hiyo kwa lengo la kujitambulisha rasmi.

Amesema ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ni lazima watendaji na viongozi waliopewa dhamana ya kuhudumia wananchi kushirikiana kwa dhati na kufanya kazi kwa weledi ili kuwatatulia kero zao za kila siku wananchi.

Aidha, ameagiza ngazi zote za uongozi kuanzia ofisi za wenyeviti wa mitaa kusimamia suala la usalama wa wananchi wao ili kuwe na amani na kujenga ari ya kufanya kazi katika nyanja mbalimbali kwenye maeneo yao ikiwemo uvuvi, kilimo na biashara.

“Ipende kazi yako, fanya kazi kwa bidii, toa huduma bora kwa jamii na tukiwahudumia vema wananchi watakua na furaha kwani matatizo yao yatasililizwa na watahudumiwa vizuri, tukumbuke kuwa mwananchi akikosa huduma atailalamikia ofisi na sio wewe uliyemkwamisha kwa kujua tu haki bila wajibu.” CPA Makalla akisisitiza juu ya uwajibikaji.

Vilevile, ameagiza Watumishi kujibu hoja za ukaguzi kwa wakati ili kuleta imani kwa wananchi na kwamba idara ya ardhi kujipanga kutimiza wajibu kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi na kutatua changamoto za ardhi kwa wananchi ili kuwa na mji uliopangiliwa vizuri.

“Moja ya maswali magumu ya Wananchi ni kwamba kwanini Mwanza iwe na shida ya Maji wakati ziwa lipo hapa jirani na huku wakiangalia Shinyanga wanapata maji kutoka hapa hivyo tuzuie upotevu wa maji kwani hiyo ni moja ya sifa mbaya sana kwahiyo lazima tuwe na mipango ya kutatua shida ya Maji kwa wananchi.” Mhe. Makalla.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema kwa mwaka 2022/23 Halmashauri hiyo imekadiria kukusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 23.6 na hadi Aprili 2023 wamekusanya kwa ziaidi ya asilimia 75 ambapo ni ongezeko kubwa lilichagizwa na mipango kazi kabambe waliyojiwekea ukiwemo upangaji wa Wafanyabiashara kwenye maeneo rasmi.

Vilevile, amefafanua kuwa kutokana na mikakati waliyojiwekea ikiwemo kuwa na timu maalum ya Ukusanyaji wa mapato hadi kufikia mwishoni mwa Juni mwaka huu Halmashauri ya jiji la Mwanza wanakusudia kufikia lengo na hata kuvuka ili kufanya vizuri kama mwaka uliopita ambao walikusanya Mapato ya ndani ya zaidi ya asilimia 105.

Aidha, Mhe. Makilagi amebainisha kuwa wamepokea fedha za Miradi ya Maendeleo kwa asilimia 77 kwani zaidi ya Shilingi Bilioni 79 zimepokelewa na kwa upande wa miradi ya kimkakati kama Meli ya MV Mwanza Bilioni 109, Ukarabati wa Meli ya MV Umoja Bilioni 19 Stendi ya Mabasi ya Nyegezi Bilioni 18 na Soko kuu la Kisasa Bilioni 17 yote inaendelea vizuri kwani wakandarasi hawadai fedha na yote ipo hatua za ukamilishaji.

Leave A Reply