RC Makalla Azitaka Halmashauri Za Ilemela Na Mwanza Jiji kuboresha mapato ya stendi za Nyamhongolo na Nyegezi
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. CPA. Amos Makalla amezitaka Halmashauri za Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza kuandaa mpango kazi wa kuboresha mapato ya Stendi za Nyamhongolo na Nyegezi na kujifunza kutoka katika Halmashauri zingine ambazo zimefanikiwa kupitia vyanzo hivyo vya mapato.
Mhe. CPA. Makalla amesema hayo wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za Mwaka 2021/22 , Juni 26, 2023.
“Angalieni vyanzo vya mapato mlivyo navyo ili mpate ushuru, wekeni huduma stahiki katika vyanzo hivyo ili muweze kuwashawishi watu Kwa vile vyanzo ambavyo vinatoa mapato navyo msimamie boresheni huduma katika masoko katika stendi ili kuhakikisha mapato yanapatikana” CPA Makalla
“Mkae muweke mkakati wa kuboresha mje na mpango kazi mzuri ndio maana nikatoa nafasi mwende mkajifunze kutoka kwenye majiji na Halmashauri ambazo zina stendi kama yenu, muwaangalie wanafanikisha vipi katika ufanisi wa stendi ili tujifunze katika manispaa zilizofanikiwa katika kuziendesha hizo stendi” amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa
Aidha, Mhe. Makalla ameitaka Menejimenti ya Halmashauri hizo kuhakikisha wanajibu hoja zote za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kuhakikisha Halmashauri inaendelea kupata hati safi.
“Leo tumekaa hapa kujadili hoja hizi ni kazi ya menejimenti mkurugenzi ukasimamie kuhakikisha hoja hizi zinatekelezwa na fanyieni kazi jibuni hoja zote kama ambavyo imeelekezwa na pale mtakapokwama msipate tabu ya namna ya kuwasiliana na ofisi ya CAG ili kupata namna ya kuziondoaha hizo hoja.
Naye, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Mkoa wa Mwanza, Waziri Shabani kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amesema kwa hesabu zinazoishia tarehe 30 Juni 2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela ilipata hati inayoridhisha.