The House of Favourite Newspapers

Makonda Aunda Kamati Kufuatilia Machinjio Vingunguti, Coco Beach

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,  leo Jumanne Septemba 17, 2019 ameunda kamati maalumu kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika mkoa huo ambayo itahusisha wataalamu mbalimbali wakiwemo maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

 

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kumwagiza Makonda kuhakikisha miradi ya ujenzi wa Coco Beach na machinjio ya Vingunguti yenye thamani ya Sh26 bilioni inakamilika kwa wakati.

 

Makonda ametoa kauli hiyo katika hafla ya utoaji udhamini kwa wanafunzi wa kike 100 wanaosoma masomo ya sayansi lakini wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha.

 

Amesema kamati hiyo itaongozwa na katibu tawala wa mkoa na itahusisha wataalamu wa sekta mbalimbali za ujenzi, ununuzi, uhasibu na maofisa wa Takukuru, kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa miradi inayoanzishwa kwenye halmashauri za Dar es Salaam.

 

“Watendaji wa halmashauri watatakiwa kutoa ripoti kwenye kamati hiyo kila baada ya wiki mbili, mara mbili kwa mwezi kwani hatuwezi kuwa tunacheleweshwa na wanasiasa kwenye halmashauri zetu,” amesema.

 

Ameongeza kwamba jana hakupata usingizi baada kumwona Rais Magufuli akizungumzia miradi ya Coco Beach na machinjio ya Vingunguti wakati kila siku anafanya vikao na watendaji wa halmashauri kuhusu miradi hiyo lakini hakuna utekelezaji wowote.

Comments are closed.