The House of Favourite Newspapers
gunners X

RC Mwassa Aongoza Dua ya Kuliombea Taifa Kata ya Katoro, Kagera

0


Dua maalum ya kuliombea Taifa iliandaliwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Farisi Buruhani, na kufanyika katika Kata ya Katoro, Halmashauri ya Bukoba, mkoani Kagera, ikiwa ni sehemu ya kumaliza mwaka kwa ibada na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Dua hiyo ilifanyika jana, tarehe 31 Desemba 2025, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatuma Mwassa. Katika hotuba yake, amewahimiza wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa mkoani humo.

Akizungumza wakati wa dua hiyo, Sheikh wa Mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta, alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na mshikamano kama nguzo ya maendeleo, huku akitoa wito kwa Watanzania kuendelea kumshukuru Mungu na kuishi kwa maadili ya kidini na kizalendo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera, Farisi Buruhani, aliwashukuru wote waliohudhuria na kusisitiza kuwa vijana wana jukumu kubwa katika kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa na mwelekeo sahihi wa maendeleo.

Dua hiyo imeonesha mshikamano wa hali ya juu kati ya viongozi wa dini, Serikali na vijana katika kujenga taifa lenye maadili, amani na maendeleo endelevu.

Leave A Reply