The House of Favourite Newspapers

Recho: Ni Mungu Tu Amenisimamia

0

WINFRIDA Josephat Mbonimpa maarufu kwa jina la Recho Kizunguzungu, ni kipaji kikubwa mno cha Bongo Fleva na Bongo Movies.

Kipaji chake kiligundulika na kukua kwenye Nyumba ya Kukuza Vipaji Tanzania (THT) chini ya marehemu Ruge Mutahaba.

 

Recho ambaye amezaliwa pacha na Wilfred, akiitwa Dotto ana sauti ya kumtoa nyoka pangoni japokuwa mwanzo alikwenda kwa nia ya kuigiza na si kuimba.

 

Recho ametamba na nyimbo kali kama Kizunguzungu, Upepo, Nashukuru Umerudi, Mwali Kigego na nyingine nyingi ambazo ziliwafanya mashabiki wake kuamini kuwa ndiye aliyekuwa anasubiriwa kuziba pengo la staa mwingine wa muziki huo, Rehema Chalamila ‘Ray C’ ambaye safari yake ya kimuziki ilitingwa na shetani wa matumizi ya madawa ya kulevya.

 

Akiwa kwenye kilele cha ustaa, ghafla Recho alipotea kwenye ramani, huku nyuma kukiwa na stori nyingi kuwa naye anapita mulemule alikopita Ray C.

Miaka miwili iliyopita, Recho alijaribujaribu kurudi kwenye mstari, lakini bado hakufikia pale mashabiki wake walipomtarajia.

 

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limepiga stori nyingi na Recho ambapo anakiri kupita kwenye changamoto nyingi za kimaisha, kiasi kwamba, ni Mungu tu amemsimamia;

IJUMAA WIKIENDA: Umekuwa kimya sana, kulikoni?

 

RECHO: Sijawa kimya sana kwa sababu mara ya mwisho nimetoa ngoma na haina muda mrefu, labda ni kwa vile tu sijatoa kazi nyingine.

IJUMAA WIKIENDA: Inasemekana umeacha muziki na kuendekeza sana starehe. Je, kuna ukweli wowote?

 

RECHO: Hapana! Si kwamba nimeacha muziki ili niendekeze starehe. Mimi kusafiri sehemu tofauti na kula bata, ni sehemu ya maisha tu. Unaweza kufanya kazi kwa muda mrefu kisha ukaamua kurefreshi kidogo na si kuendekeza starehe.

 

IJUMAA WIKIENDA: Kwa upande wako, unaizungumziaje Corona kama msanii na imekuathiri vipi?

RECHO: Kila mtu inamuathiri hasa sisi wasanii. Kwa sasa shoo zimesimama; hatuna jinsi, ni kusubiri tu janga lipite maana linaathiri Taifa na dunia kwa ujumla.

 

IJUMAA WIKIENDA: Mipango yako ya kutoa kazi mpya ikoje?

RECHO: Mipango ni kutoa kazi nyingi na ziwafikie mashabiki, ila nasubiri kwanza Corona lipite.

IJUMAA WIKIENDA: Kwa upande wako unaizungumziaje THT kama sehemu iliyokulea na ukakua kimuziki?

 

RECHO: THT itabaki kuwa THT, maana ni sehemu ambayo imenitoa na kunikuza na bado kuna vipaji vingi ambavyo vinaendelea kufanya vizuri.

IJUMAA WIKIENDA: Inasemekana tangu uanze muziki, umekuwa ukiiga swaga za Ray C kwa kila kitu. Je, ni kweli?

 

RECHO: Hapana, sidhani kama kuna mtu anaweza kuiga kila kitu cha mtu na akakifanya kama mhusika. Nadhani ni jinsi tulivyofanana tu ndiyo maana huwa watu wanazungumza hivyo.

IJUMAA WIKIENDA: Je, una mpango wa kufanya kazi ya pamoja na Ray C?

 

RECHO: Tulishafanya kazi mbili ambazo bado hazijatoka, mashabiki wategemee kuziona japo tumeshindwa kuendelea kutoa kazi za pamoja kwa sababu mwenzangu yupo mbali (Uingereza).

IJUMAA WIKIENDA: Katika ngoma zako ambazo umetoa, ni ipi unaishi nayo mpaka sasa?

 

RECHO: Nina ngoma nyingi nzuri, ila Upepo na Nashukuru Umerudi ni ngoma ambazo nazikubali na ninaishi nazo.

IJUMAA WIKIENDA: Vipi kuhusiana na kolabo za kimataifa?

RECHO: Zitakuja tu japo bado hazijakuwepo, hiyo ni ndoto ya kila msanii.

 

IJUMAA WIKIENDA: Kwa sasa muziki umekuwa na ushindani hasa kwa watoto wa kike, kwa upande wako unalinda vipi kipaji chako?

RECHO: Kipaji cha mtu hakipotei, kama kipaji changu kipo, basi kitaendelea kudumu japokuwa ni kweli kwa sasa kumekuwa na wingi wa wasanii wa kike wanaofanya vizuri na kazi zao zinaonekana.

IJUMAA WIKIENDA: Zilikuwepo tetesi kuwa ulijiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, umeacha?

 

RECHO: Huwa sipendi kulizungumzia suala hilo.

IJUMAA WIKIENDA: Ni changamoto gani umepitia kwenye muziki wako?

RECHO: Changamoto ni nyingi sana hadi kufika hapa nilipofika. Kikubwa niseme wazi kwamba, ni Mungu tu amenisimamia.

 

IJUMAA WIKIENDA: Kila kazi ina mafanikio yake. Je, ni mafanikio gani unajivunia katika kazi yako?

RECHO: Mafanikio yapo hata kama si makubwa sana, lakini nashukuru Mungu kipo ambacho najivunia.

 

IJUMAA WIKIENDA: Je, vipi kuhusiana na mipango ya ndoa au mtoto?

RECHO: Natamani sana kuwa na mtoto maana umri nao unakwenda, Mungu asaidie tu.

IJUMAA WIKIENDA: Unatamani upate mtoto wa aina gani?

 

RECHO: Natamani Mungu anipe mtoto wa kike; yaani nitafurahi sana.

IJUMAA WIKIENDA: Ulisikika ukisema kuwa hupendi mwanaume ambaye hajielewi, ulimaanisha nini?

RECHO: Ni kweli sipendi mwanaume mhuni ambaye hajielewi, sharobaro tu ambaye hata hafanyi maendeleo, huyo hawezi kuwa baba bora.

 

IJUMAA WIKIENDA: Mbali na muziki, una kipaji gani kingine?

RECHO: Mimi ni mwigizaji mzuri, maana hata kabla ya kuingia kwenye muziki, nilikuwa naigiza. Hata THT nimeenda kama mwigizaji.

MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA

Leave A Reply