The House of Favourite Newspapers

Rigwaride Ra Afande – 17

0

ILIPOISHIA RISASI JUMATANO:

Mwezi mmoja ulikatika bila kupata mawasiliano kutoka kwa yeyote kati yao. Lakini siku hiyo niliamka ninaumwa. Afya haikuwa njema. Nilipokuwa najisaidia, nilisikia maumivu makali sana, halafu sehemu ya chini ya tumbo ikawa inauma pia…
“Mama,” nilimwita…

JIACHIE MWENYEWE…

“Nini?” mama aliniitikia kindava. Eti nini!
“Naumwa mama…tumbo linaniuma, hapa chini linauma sana,” nilimwambia mama baada ya kuja.
“Ni kwa sababu gani?”
“Sijui mama,” nilisema nikijishika tumbo kwa maumivu…
“Lakini wakati nimekwenda chooni nilihisi haja ndogo yangu ina rangi ya maziwa,” nilimwambia mama…
“Hee! Twende hospitali haraka sana. Jiandae,” alisema mama na kunipa hofu kwani niliamini mshtuko wake una jambo alilolijua.
Nilijiandaa harakaharaka, nikamwambia mama, tukaondoka hadi Hospitali ya Temeke. Mimi wasiwasi wangu mkubwa nimenasa ujauzito. Nikawa najiuliza kama ni kweli ni wa nani sasa..?
“Itakuwa Afande Mwira? Mh! Sidhani, labda afande Mwita…lakini yule siyo, ila itakuwa afande Chacha yule mbaba.”
Niliwaza mengi mpaka ikafika mahali nikawa nasubiria niingie kwa dokta na kuambiwa maelekezo.
Daktari alikuwa amekaa kwenye kiti chake miwani usoni wakati mama akimsimuliza matatizo yangu, ninavyojisikia.
Vipimo vilichukuliwa kwa kuambiwa nikajisaidie haja ndogo. Nilipomaliza, nikawapa kikopo kisha tukaambiwa tukae nje. Mama hakuonekana mwenye raha sana. Kila mara aliniangalia kwa kuibia.
“Rhoda…” aliita daktari kabla hata hajamalizia jina la baba, nikawa nimeitika, tukaenda na mama…
“Karibuni sana,” alisema daktari…
“Eee…kipimo tayari…eee! Kipimo chetu kinaonesha Rhoda umeambukizwa ugonjwa wa zinaa.”
Palepale mama aliangua kilio, mimi nikafuatia…
“Sasa hapa…sasa hapa si mahali pa kumalizia vilio vyetu. Tunaruhusu kulia kwa mtu aliyefiwa tu. Haya ni matatizo ya kujitakia, msinipigie kelele,” alisema yule daktari huku akiniandikia dawa…
“Itabidi uchome sindano za PPF tatu kwa siku tatu na utumie dawa inayoitwa Azithromycin. Fuata maelekezo tafadhali,” alisema dokta huku akiniangalia kwa macho makavu.
Tulitoka na mama tukiwa tumeinamisha vichwa chini. Nilijiuliza kisa cha mama kulia ni nini! Nilitarajia baada ya maelezo ya daktari palepale angenishika masikio yangu na kuyang’ata lakini sivyo…
“Mwanangu Rhoda nisamehe mimi…nisamehe sana mwanangu. Mimi ndiyo sababu ya wewe kuupata huo ugonjwa, nisingekuacha naamini yasingekukuta,” alisema mama mpaka nikamshangaa…
“Usijali mama…Mungu atanisaidia mama. Nitapona tu,” nilimwambia mama…
“Sawa mwanangu, lakini lazima twende kwa yule askari tukamwambie, lazima atoe pesa za kukutibu. Leo atanitambua mimi ni nani!” mama alikuja juu.
Nilimkubalia mama kwenda kwa wale maafande lakini yeye akijua ni afande mmoja tu. Moyoni nilisema hata kama nitakwenda kuumbuka lakini yote aliyataka mama na ameshakiri mwenyewe.
Tulikata mitaa, tukachanja uchochoro mpaka tukatokea kwenye ile nyumba na kuwakuta wanawake wawili nje, mmoja akichagua mchele. Kwanza nilishtuka sana, nikajua wale wanawake ni wake wa wale maafande. Nilitaka kumwambia mama lakini hakuonesha dalili ya kunisikiliza…
“Hodi hapa,” alisema mama akiwa amenishika mkono…
“Karibuni,” tulipokelewa…
“Tunamuulizia askari mmoja anaitwa…eti wewe anaitwa nani yule askari wako?” mama alisema, akaniuliza mimi.
Kutaja jina nilishindwa, nilijua kama ana mke kati ya wale, itakuaje sasa! Si nitakula kichapo?! Nikakaa kimya!
“Wewe si nakuuliza?” mama alinijia juu…
“Anaitwa afande Mwira,” niliamua kumtaja yule wa kwanza kabisa.
Wale wanawake waliangaliana, kisha mmoja akasema…
“Hapa wamekuja askari wapya! Wale wa zamani wote wamehamishwa! Si mnajua polisi hawakai sehemu moja kwa muda mrefu!”
Nilimwangalia mama, naye akaniangalia mimi…
“Kwa hiyo na nyinyi ni maaskari?” aliuliza mama…
“Hapana, sisi ni wake zao.”
Mama alinishika mkono tukageuza kuondoka…
“Kwani kuna nini mama?”
“Ah! Basi! Mungu atatulipia,” alisema mama tukiwa tunakata kona kuingia kwenye uchochoro.
Tulifika nyumbani na kukaa kwenye mkeka, mama alilia na mimi nililia. Mimi nililia kwa sababu niliamini niko kwenye starehe kwa sababu ya ujana wangu na uzuri lakini kumbe nachuma janga sasa nakula na wa nyumbani.
Nilijuta kuutumia mwili wangu vibaya. Nilijuta kutotumia akili yangu kujiongeza kwamba, natakiwa kutulia. Kama ni boifrendi nilikuwa naye, sasa kwa nini nilizama kwenye mapenzi ya mchanyato!
“Rhoda,” aliniita mama…
“Abee mama.”
“Tulia mwanangu, utapona na Mungu atakusaidia.”
“Natulia mama. Nakuahidi kuanzia leo, tena kuanzia sasa, mimi nimetulia mama.”
Mama alinifuata, akanikumbatia, tukakumbatiana!

MWISHO.

Leave A Reply