The House of Favourite Newspapers

Rihanna ‘The Bad Gal’ Uhuni, Usela Vinampa Mkwanja Mnono

0
Rihanna.

 

UKIMTAZAMA mwonekano wake jinsi alivyo mrembo, mwenye haiba nzuri ya kike, mvuto wa asili na sauti yenye utamu wa aina yake, huwezi kumdhania kwamba nyuma ya pazia ni mhuni na ‘msela’ aliyepitiliza!

Jina lake halisi anaitwa Robyn ‘Rihanna’ Fenty, anapenda zaidi ukimuita Riri au The Bad Gal, mwanadada asiyechuja kutoka Visiwa vya Barbados, anayefanya poa kinoma kwenye anga la muziki wa kimataifa, maskani yake yakiwa nchini Marekani.

Jina lake ni miongoni mwa wasanii wachache wa kike wanaoitingisha dunia kwa sasa, akichuana vikali na Beyonce Knowles, ingawa wapo baadhi ya watu wanaosema si sahihi kuwapambanisha wawili hao kwani Beyonce ni mkongwe na ana mafanikio zaidi ya Rihanna.

Miongoni mwa matukio ya hivi karibuni yanayodhihirisha jinsi Rihanna ‘alivyopinda’, ni kwenye video ya Wimbo wa Wild Thoughts wa DJ Khaled, akiwa amemshirikisha mwanadada huyo na chalii mwingine, Bryson Tiller.

Ukiisikiliza ngoma hii iliyoachiwa mwishoni mwa mwezi uliopita, Juni, 2017, ikiwa ni miongoni mwa ngoma nyingine kadhaa zilizomo kwenye albamu ya Grateful ya DJ Khaled, utakubaliana nami kwamba Rihanna amefanya maajabu ya kimuziki.

Amefanya kile ambacho alitarajiwa na wengi, amekamua kwa uwezo wake wote kiasi kwamba unaweza kudhani kwamba yeye ndiye mwenye wimbo! Ni hapo ndipo unapoweza kuelewa ni kwa nini DJ Khaled alifurahi sana siku Rihanna alipokubali kufanya naye ngoma hiyo.

Rihanna.

 

 

Pamoja na kazi kubwa aliyoifanya kwenye ‘audio’ ya wimbo huo, ukitazama video yake, hasa ukimtazama Rihanna mwenyewe, hakika huwezi kurudia tena kutazama video hiyo ukiwa sebuleni na watoto, wakwe au ukiwa na watu unaowaheshimu.

Video hiyo inapoanza, Rihanna anaonekana akiwa anaingia klabu akiwa na DJ Khaled, kinguo alichovaa upande wa kifuani, kinaacha kila kitu wazi kabisa utafikiri hajavaa chochote. Hali inaendelea hivyo karibu video nzima, Rihanna anabadilisha nguo mara kadhaa lakini zote ni zile za kihasarahasara, zinazomuonesha mubashara maungo yake nyeti!

Unaweza kudhani ni bahati mbaya lakini ukweli ni kwamba huu umekuwa mchezo wa Rihanna kwa kipindi kirefu sasa, tazama video yake ya Work iliyomo kwenye albamu yake ya nane, Anti aliyoitoa mwaka jana (2016), akiwa na Drake! Laana tupu.

Ukifuatilia karibu video zote za Rihanna, kuanzia Pon De Replay iliyomtambulisha mpaka Diamonds, American King Bed na nyingine kibao, kuonekana akiwa kwenye mapozi yenye ‘amshaamsha’ za hatari na pozi tata, ni kama jadi yake.

Rihanna na Drake.

 

Ukiachilia mbali suala hilo, katika video zake nyingi, ni jambo la kawaida kabisa kumuona akila majani (akivuta bangi), akijidunga madawa ya kulevya, akionesha ishara za mapenzi ya jinsia moja (usagaji) kama ilivyo kwenye Te Amo, Disturbia, Where Have You Been na nyingine nyingi!

Kuonekana akifanya matendo ya kihalifu kama kumtwanga risasi mwanaume aliyemnyanyasa kimapenzi kama anavyoonekana kwenye Man Down, kuonekana akiabudu dini ya shetani, akifanya ngono hovyo na uchafu mwingine mwingi, ni kama tabia yake kwenye gemu, imemkaa damuni na hata mashairi na video zake zinazungumza hivyo.

 

Licha ya kwamba ni ‘demu mkali’, Rihanna ni mhuni na ‘gangstar’ aliyepitiliza kwenye kazi zake, sijui kuhusu maisha yake binafsi lakini cha ajabu sasa, uhuni, uchakaramu, umapepe na kujichetua kulikopitiliza, ndiko kunakomfanya aendelee kuwa juu kila kukicha.

Kwa mujibu wa mitandao kadhaa inayoongoza kwa kuandika habari za mastaa wakubwa Marekani na duniani kote, mashabiki wengi wa Rihanna wanavutiwa na ‘swaga za kihuni’ anazozionesha kuanzia kwenye mashairi yake mpaka video zake kiasi kwamba hawaambiwi wala hawasikii kuhusu mwanadada huyu!

 

Rihanna.

 

Wanampenda tu vile alivyo na mara kwa mara msuguano mkali wa mashabiki wanaomkubali na wale wanaomkubali hasimu wake kimuziki, Beyonce Knowles, umekuwa ukiibuka na kusababisha taharuki kubwa, kila upande ukiamini msanii wao ndiye mkali zaidi!

Beyonce anao mashabiki wake ambao wengi ni watu na heshima zao lakini Rihanna, mashabiki wake ni kutoka kila kada, wapo watu na heshima zao, wakubwa kwa wadogo lakini wengi ni masela na wahuni, achilia mbali masistaduu! Uhuni wake unawakuna wengi ndiyo maana wanamuunga mkono kwa kila anachokifanya, bila kujali ni kizuri au kibaya.

Kwa taarifa yako tu, licha ya ‘usela’ anaouonesha, Rihanna anazidi kutusua kila kona, anatisha kwenye muziki, ameshafanya poa kwenye muvi na sasa anakimbiza kwenye ulimwengu wa fasheni na ubunifu wa mitindo ya nguo na viatu, akiwa amesaini mkataba mnono na Kampuni ya Puma kutoa ingizo jipya la viatu vyake viitwavyo Fenty Puma Creeper!

Anapiga tu mkwanja licha ya uhuni wake!

Na Hashim Aziz kwa msaada wa mitandao.

New York, Marekani

Leave A Reply