The House of Favourite Newspapers

Ripoti Kifo cha Kabote, Wafungwa Kutoroka Zatua kwa Lugola

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amepokea ripoti mbili za uchunguzi ikiwemo ya kifo chenye utata cha Isululu Kabote (85), mkazi wa Kijiji cha Buhungukila, Kata ya Bugarama, Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu.

 

Kabote alidaiwa kuuawa akiwa mikononi mwa polisi Mei 17, mwaka huu, saa 8:00 usiku. Pia Lugola alipokea ripoti ya uchunguzi wa tukio la kutoroka mahabusu 17, Mei 21, mwaka huu, mkoani Geita.

 

Mahabusu hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali na kuwekwa kwenye Ukumbi wa Jengo Jipya la mahakama wakisubiri kusomewa kesi zao.

 

Ripoti ya uchunguzi wa kifo cha marehemu Kabote iliwasilishwa na Lalph Meela (Mwenyekiti), kutoka Dawati la Malalamiko Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

Wajumbe ni Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Ibenze Ernest, Kefa Kaswamila kutoka Dawati la Malalamiko Kitengo cha Upelelezi Wizara ya Mambo ya Ndani na Mzee Mzee kutoka Ofisi ya Ofisa Usalama, Mkoa wa Simiyu.

 

Kamati hiyo ilifanya uchunguzi huo kuanzia Juni 4-10, mwaka huu ambapo ripoti ya uchunguzi wa tukio la kutoroka wafungwa ilikabidhiwa na Mwenyekiti wake, Alex Mfungo.

 

Baada ya kupokea ripoti hizo, Lugola alisema ameridhishwa na matokeo ya uchunguzi huo ambapo wajumbe wa kamati zote walipata fursa ya kuzichambua ripoti hizo sambamba na kutoa mapendekezo.

 

Viongozi wengine waliokuwepo wakati Lugola akipokea ripoti hizo ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali, Jacob Kingu na Naibu Katibu Mkuu, Ramadhani Kailima.

 

Kamati ya uchunguzi wa kifo cha Kabote iliundwa baada ya wananchi wa kijiji hicho kudai kabla ya kukumbwa na mauti, alikamatwa na polisi, kupigwa akidaiwa hajatoa mchango wa maendeleo sh. 50,000 madai ambayo Jeshi la Polisi liliyakanusha.

 

Mmwili wa marehemu Kabote ulikaa siku 20 katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya uchunguzi wa kidaktari.

Na Veronica Mwafisi, MOHA

Comments are closed.