The House of Favourite Newspapers

Ripoti ya Mali za CCM Yatua Mikononi mwa JPM, Atoa Kauli – Video

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli leo Mei 21, 2018 amepokea ripoti ya tume aliyoiunda kuhakiki mali za chama, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa tume hiyo Dkt. Bashiru Ally Kakurwa katika ofisi ndogo ya CCM Lumumba Jijini Dar es Salaam.

 

Kamati hiyo imefanya kazi kwa miezi mitano ambapo imekusanya, imehakiki na kuchambua taarifa na nyaraka zenye maelezo kuhusu idadi, aina na hali ya mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na chama, imeangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wa mali, imekusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya mikakati na ushauri wa kusimamia mali za chama.

 

Aidha, Dkt. Magufuli ameipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na kusema ripoti hiyo itawasilishwa katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.

 

“Nilipokuwa nateua tume hii nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki sasa ni kuifanyia kazi” amesema Rais Magufuli.

 

Mbali na hilo Rais Magufuli amewaagiza wajumbe wa sekretarieti ya CCM waliohudhuria wakati wa uwasilishwaji wa ripoti hiyo kuanza kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na kwamba masuala mengine yataamuliwa na vikao vikuu vya chama.

 

Kabla ya kuondoka katika ofisi ndogo za CCM Lumumba, Dkt. Magufuli amesalimiana na wananchi waliokuwa nje ya ofisi hiyo na kuwahakikishia kuwa CCM imeamua kuhakiki mali zake ili kukiwezesha chama hicho kulinda mali zake na kunufaika na mali hizo.

 

“CCM imeamua kuchukua hatua hii ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya kupiga vita rushwa na ufisadi, huwezi ukaanza kupiga vita rushwa na ufisadi ndani ya Serikali wakati chama kina rushwa na ufisadi, chama nacho tunataka tukisafishe, mambo ya rushwa na ufisadi yaishe ili Tanzania iende vizuri, ndio maana tumeunda tume ya Dkt. Bashiru Ally, imefanya kazi nzuri sana, na ripoti hii tutaipeleka Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ndani ya mwezi huu ili tuijadili na viongozi watoe maelekezo” amesisitiza Rais Magufuli.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa tume hiyo Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema katika ripoti yake tume imebaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibaya, ubadhilifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama.

Comments are closed.