The House of Favourite Newspapers

Ronaldo Aanza Na Hat Trick Urusi

Cristiano Ronaldo

 

CRISTIANO Ronaldo alianza kwa kishindo Fainali za Kombe la Dunia baada ya kupiga mabao matatu yaliyosaidia timu yake ya Ureno kutoka sare ya mabao 3-3 na Hispania katika pambano kali la Kundi B lililochezwa usiku wa kuamkia leo Jumamosi mjini Sochi.

Pambano hilo lililokuwa linasubiriwa kwa hamu kwa kuwa lilikuwa na mambo mengi kwani Ronaldo, alikuwa anacheza dhidi ya nchi ambayo wanatokea waajiri wake, Real Madrid na pia vigogo Hispania na Ureno ni majirani barani Ulaya.

Kufuatia sare hiyo, timu hizozimegawana pointi na kutakiwa kupatamatokeo mazuri dhidi ya Morocco na Iran ili kukata tiketi ya kucheza kwenye mtoano.

 

Ronaldo, mwenye umri wa miaka 33, ambaye wadau wengi wa soka wanaamini ndio zitakuwa fainali zake za mwisho, aliifungia timu yake mapema dakika ya nne kwa njia ya penalti. Penalti hiyo ilisababishwa na beki wa Hispania, Nacho, ambaye alimfanyia rafu Ronaldo kwenye eneo la penalti kufuatia presha ya Ureno katika dakika za mwanzo.

 

 

Bao hilo liliizindua Hispania, ambayo ilianza kwa kusuasua ukizingatia imo kwenye msukomsuko kufuatia kutimuliwa kwa kocha wake Julen Lopetegui, siku chache kabla ya mechi ya jana.

Hispania ilianza kumiliki mpira zaidi na kuonyesha uelewano na ingeweza kusazawazisha katika dakika ya 16 baada ya shuti kali la David Silva kugonga mwamba kufuatia kazi nzuri ya Andres Iniesta kwenye wingi ya kushoto.

 

Presha ya Hispania ilisababisha Ureno kurudi nyuma kujihami na ilizaa matunda katika dakika ya 24 baada ya Diego Costa kusawazisha kufuatia kumzidi nguvu beki mtata wa Ureno, Pepe na kupiga shuti kali lililotinga wavuni.

 

Bao hilo liliwavuruga Ureno lakini ilipata bahati baada ya kupata bao la pili mnamo dakika ya 44 baada ya kipa wa Hispania, David De Gea kutema wavuni shuti kali la Ronaldo.

Hata hivyo, kibao kiligeuka kipindi cha pili kwani Hispania ikicheza soka la pasi za hatari ilipata mabao mawili katika muda wa dakika tatu.

 

Costa aliifungia Hispania bao la pili katika dakika ya 55 baada ya kuweka mpira wavuni kwa shuti la karibu baada ya kuunganisha pasi ya kichwa ya Sergio Busquets.

 

 

Nacho naye alifuta makosa yake ya kusababisha penalti baada ya kufunga bao la tatu la Hispania katika dakika ya 58 kwa shuti kali la nje ya eneo hatari lililofonga mwamba na kuingia wavuni.

 

Hata hivyo wakati kila mtu akiamini Ureno ilikuwa imelala na ukizingatia ilicheza ovyo katika kipindi cha pili lakini dakika ya 88, Ronaldo aliisawazishia Ureno kwa mpira maridadi wa faulo.

 

 

Katika hatua nyingine, wawakilishi wa Afrika, Misri na Morocco kwenye fainali hizo walianza vibaya jana baada ya wote kujikuta wakifungwa bao 1-0 katika dakika za lala salama.

 

 

Misri ililala kwa Uruguay kwa bao lililofungwa katika dakika ya 90 na Jose Gimenez katika mechi ya Kundi A wakati bao la kujifunga la Aziz Bouhaddouz lilisaidia Iran kuibuka na ushindi kwenye mechi ya Kundi B.

Comments are closed.