The House of Favourite Newspapers

RONALDO, HISPANIA VITANI KUSAKA TIKETI YA MTOANO

CRISTIANO Ronaldo akiongoza timu yake ya Ureno na Hispania zina kibarua kizito cha kufungua njia ya kufuzu kwa hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia kutoka Kundi B.

 

Baada ya kugawana pointi, Ureno na Hispania sasa lazima zishinde mechi zao za leo Jumatano ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele kutoka katika Kundi B.

 

URENO V MOROCCO

Ureno, ambayo ni bingwa wa Ulaya itakabiliana na Morocco, ambayo katika mchezo wa kwanza ililala bao 1-0 kwa Iran.

Ronaldo atakuwa anaongoza kikosi chake ili kuhakikisha kinaondoka na ushindi katika mchezo huu ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele kutoka katika Kundi B.

 

Morocco, ambayo haina pointi ili kuvuka hatua ya makundi, ushindi ni lazima baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Iran, ambao kimsingi ulitakiwa ndiyo ungekuwa mteremko kwao.

 

Hata hivyo, Morocco itajipa moyo kuwa inaweza kufanya maajabu kama yale ya mwaka 1986 wakati ilipoicharaza Ureno mabao 3-1 na kuvuka kutoka katika kundi lake.

 

Ni mwaka huo wa 1986, wakati Morocco ilipokuwa na kikosi cha hatari kilichokuwa kinaongozwa na Mohamed Timmoumi, Aziz Bouderballa, Abdurazak Khairy na kipa Badou Zaki ndiyo kiliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kuvuka makundi na kuingia kwenye mtoano.

 

Morocco, ingawa ina mlima mrefu wa kupanda kwani itapaswa kuwa na mbinu ya kumbana straika hatari wa Ureno, Ronaldo, ambaye alifunga mabao matatu wakati timu yake ilipofungana mabao 3-3 na Ureno.

Pia katika mchezo wa kwanza, ambao Morocco walipoteza kwa Iran, walimiliki mpira kwa muda mrefu lakini tatizo kubwa lilikuwa umaliziaji.

 

Pamoja na kuwa Iran haikupiga hata shuti moja katika kipindi cha pili cha mchezo dhidi ya Morocco, lakini bado iliweza kuibuka na ushindi.

Hata hivyo, ukweli unabakia kuwa Ureno ni jeshi la mtu mmoja wakimtegemea staa wao, Ronaldo.

Ronaldo alizamisha mabao 15 katika mechi tisa za kuwania kufuzu kwa fainali hizo na alidhihirisha makali yake kwa kupiga`hat-trick’ kwenye mechi dhidi ya Hispania.

Kikosi cha Morocco hakitakuwa na mabadiliko makubwa kwenye mchezo huu wa pili licha ya kupoteza mechi ya kwanza.

 

Hata hivyo, wanakabiliwa na changamoto ya kukabiliana na tatizo la ukame wa mabao kwani kwa mfano katika mechi dhidi ya Iran walimiliki mpira kwa asilimia kubwa.

 

Ureno inatazamiwa kutumia fomesheni ya 4-4-2 ikiwa na kazi moja tu ya kupata ushindi ingawa inahitaji mbinu ya kuhakikisha inapunguza kumtegemea Ronaldo.

 

Morocco nayo inatazamiwa kutumia mfumo wa 4-2-3-1, ambao ilitumia kwenye mechi ya kwanza.

Hata hivyo, huenda wakabadili mfumo na kucheza 4-3-3 ili kuipa wakati mgumu beki ya Ureno.

HISPANIA V IRAN

Hispania nayo itakabiliana na Iran huku mtu atakayekuwa anaangaliwa zaidi ni kipa David de Gea.

De Gea, ambaye alikuwa kipa bora msimu huu wa Ligi Kuu England, alifungisha kwenye mechi ya Hispania baada ya kutema wavuni shuti la Ronaldo.

Pia alifungwa na Ronaldo bao la faulo baada ya kuwa ameachia nafasi katika ukuta wake.

Ingawa watu wanakuwa wepesi wa kusahau kuwa umahiri wake kwa kiasi kikubwa ulisaidia timu hiyo kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia.

Kocha wa Hispania, Fernando Hierro ameshikilia kuwa De Gea ataendelea kukaa golini licha ya kuboronga kwenye mechi dhidi ya Ureno.

Hispania bado inapewa nafasi kubwa ya kushinda katika mechi hiyo dhidi ya Iran itakayochezwa Kazan, ambako inasaka ushindi wa kwanza.

Iran itajipa moyo kuwa nayo ina nafasi ya kuibuka kidedea baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Morocco, wiki iliyopita.

Kipa wa Iran, Alireza Beiranvand amejigamba kuwa baada ya timu yao kuibuka kidedea kwenye mechi ya kwanza wako tayari kwa pambano gumu dhidi ya Hispania.

“Kila mtu anajua Hispania ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa Kombe la Dunia. Ila sisi ni wapiganaji na kimsingi tutapigana kufa na kupona ili kupata ushindi,” alisema kipa huyo.

Hispania inatakiwa kumchunga staa wa Iran, Sardar Azmoun, ambaye anachezea Rubin na alikuwa tishio kwenye mechi dhidi ya Morocco.

Iran itatakiwa kuwa katika kiwango bora ili kupata ushindi kwenye mechi dhidi ya Hispania.

Straika wa Hispania, Diego Costa aling’ara kwenye mechi dhidi ya Ureno kwa kufunga mabao mawili lakini Iran watapaswa kumwangalia sana Isco kwani ndiye mpishi mkuu wa mashambulizi ya Hispania.

Iran, hata hivyo, ina rekodi mbovu dhidi ya timu za Ulaya, ambapo kwenye Kombe la Dunia imepigwa mechi sita.

Hispania nayo imekuwa na rekodi yenye mkanganyiko kwenye fainali hizi kwani katika fainali tatu zilizopita haikushinda mechi yao ya mwanzo.

Comments are closed.