RONALDO NI HABARI NYINGINE, AISAMBARATISHA ATLETICO KWA HAT-TRICK

DUNIA nzima inatambua ubora wa mshambuliaji wa Juventus, Cristiano Ronaldo na hakuna ambaye alishangaa kwa kile alichofanya usiku wa kuamkia leo kwenye Dimba la Allianz nchini Italia.

 

Juventus kwenye mchezo wa kwanza waliocheza nchini Hispania wiki tatu zilizopita walichapwa mabao 2-0 na Atletico Madrid katika mechi ya hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini jana Ronaldo alipiga mabao matatu ‘hat trick’ na kuipeleka Juventus robo fainali.

Ronaldo ambaye ameshatwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia mara tano, alifunga mabao hayo kila kipindi na kuipa timu yake ushindi wa mabao 3-0, ikatinga robo fainali kibabe.

Ronaldo ambaye ameshatwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne, alifunga mabao yake yote mawili ya kwanza kwa kichwa, alifunga la kwanza katika dakika ya 27 na bao la pili katika dakika ya 48 ya mchezo huo.

Hata hivyo, wakati Atletico wakipambana kurudisha, Juventus walipata penalti dakika ya 86 ambapo Ronaldo alichukua mpira na kuweka kimiani bao la tatu kwa timu yake na yeye akiondoka na mpira usiku huo baada ya kufunga hat-trick yake ya kwanza msimu huu kwenye Uefa na kuwafanya wafuzu kwa jumla ya mabao 3-2.

Huu ndiye mchezo wa kwanza ambao Ronaldo ameonyesha Kiwango cha hali ya juu sana msimu huu kuanzia alipojiunga na Juventus mwishoni mwa msimu uliopita akitokea Real Madrid.

Hii ni picha halisi kuwa staa huyo anaweza kutwaa tena tuzo ya mchezaji bora wa dunia mwakani.

MAN CITY NAO WAFUZU

Manchester City ambao wamekuwa wakiutafuta ubingwa huu kwa muda mrefu bila mafanikio jana walifanikiwa kufuzu kwenda robo fainali baada ya kuwachapa Wajerumani, Schalke 04, mabao 7-0.

Awali City walishinda kwa mabao 3-2 ugenini, lakini jana wakiwa nyumbani kwenye Dimba la Etihad, walionyesha kiwango cha hali ya juu na kupata ushindi huo mnono.

Sergio kun Aguero alikuwa shujaa kwenye timu hiyo baada ya kufunga mabao mawili katika dakika ya 35 kwa mkwaju wa penalti na 38.

Mabao mengine ya City ambao wanaongoza kwenye Ligi Kuu England yaliwekwa kimiani na Sané (43), Sterling (56), Bernardo Silva dakika ya 71, Foden aliyefunga la sita dakika ya 78 na Jesus akafunga kitabu dakika ya 84 na kuwafanya City wafuzu kwa jumla ya mabao 10-2.

City imekuwa timu ya kwanza kupata ushindi mnono zaidi kwenye hatua ya 16 Bora msimu huu. Sasa inamaana kuwa City imeungana na Ajax, Manchester United, Juventus, Porto na Tottenham kwenda hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya.

Wanachama Yanga watoa Kauli kwa Wanaokwamisha Uchaguzi

Toa comment