The House of Favourite Newspapers

Rose Muhando, MSHUKURU MUNGU, CHUNGA SANA USIRUDI ULIKOTOKA

SIKU chache zilizopita, picha zinazomuonesha mwimbaji mahiri wa nyimbo za Injili, Rose Muhando akiwa amenawiri na kupendeza, ziliibua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii. Rose huyu wa sasa, si yule wa miezi kadhaa iliyopita, si yule wa miaka michache iliyopita, Mungu ametenda!

 

Unaweza kumfananisha na ‘mfu’ aliyerejewa na uhai! Ndiyo, Rose Muhando ‘amefufuka’ kutoka katika wafu. Kwa wanaomjua vizuri mwimbaji huyu wa Injili, watakuwa wananielewa vizuri ninachokimaanisha.

Kwa miaka mingi Rose Muhando alikuwa amepoteza mwelekeo, kelele zilizokuwa zinapigwa dhidi yake zilikuwa nyingi mno, tuhuma na kashfa zilizokuwa zinamkabili, zilikuwa nzito kwelikweli, ikiwemo ile ya kujidunga madawa ya kulevya.

 

Si lengo langu kuzungumzia kuhusu mapito aliyopitia Rose Muhando kwa sababu Waswahili wanasema (ashakum si matusi), mavi ya kale hayanuki! Lakini kwa kuwa sasa amerejea kwenye mstari, ni vyema kumkumbusha baadhi ya mambo ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yaliyomfanya akaangukia shimoni.

Kwa wasiofahamu alikotokea Rose Muhando, mwanamama huyu ni mzaliwa wa Morogoro mwenye makazi yake Dodoma. Nyota yake ilianza kung’ara mwanzoni mwa miaka ya 2000, akiwa na Kwaya ya Kitimtimu ya Kanisa la Kianglikani la Chimuli mkoani Dodoma.

 

Akiwa kwenye kwaya hiyo, uwezo wake ulijidhirisha na hapo ndipo alipoonwa na Nathan Wami ambaye amekuwa meneja wake kwa miaka kibao. Nathan ndiye aliyemuingiza Rose Muhando kwenye uimbaji wa ‘gospel’ kama msanii wa kujitegemea.

Albamu yake ya kwanza kama mwimbaji Injili wa kujitegemea, ilikuwa ni Uwe Macho, aliyoitoa mwaka 2004 na hapo ndipo Rose Muhando unayemjua wewe, alipoanza kutambulika nchi nzima na Afrika Mashariki kwa jumla.

 

Sauti yake ya kipekee, uwezo wa kuandika mashairi yenye ‘upako’, na uchangamfu wake awapo jukwaani, zilikuwa ni baadhi ya sifa zilizolifanya jina lake lipae kwa kasi ya kimbunga, kila mtu akamtambua na kumsifia, kila mtu akawa anaimba nyimbo zake, maisha yake yakabadilika kabisa.

Hata hivyo, wakati akiwa kwenye kilele cha mafanikio yake, upande wa pili wa maisha yake, Rose alikumbwa na ‘pepo mchafu’. Rose alianza kutuhumiwa kuingia mitini na fedha alizokuwa akipewa kwa ajili ya kufanya matamasha, ikawa kila siku ni kesi.

 

Baadaye likaja kuibuka suala zito kwamba mtumishi huyo wa Mungu anayefanya kazi ya kutangaza Injili kupitia uimbaji wake, alikuwa akitumia madawa ya kulevya. Japo alijitahidi kukanusha, mwonekano wake na matendo yake vilidhihirisha waziwazi kwamba alikuwa akijidunga!

Mwisho akapoteza kabisa mwelekeo, kipaji kikapotea, maisha yake yakawa hayaeleweki, ikawa madawa na yeye, yeye na madawa!

 

Simlaumu sana kwa aliyopitia kwa sababu ukichunguza kwa makini, kuna ‘rafu’ nyingi alikuwa akichezewa, ambazo ndizo zilizomsababisha akakumbwa na msongo mkali wa mawazo, uliompeleka mpaka kwenye janga la matumizi ya madawa ya kulevya.

Video ya mwisho iliyogusa hisia za watu wengi, ilikuwa ni ile iliyomuonesha Rose akiwa amechakaa, ana makovu mwili mzima, ana majeraha, amepauka na kuchoka, akiombewa na Pastor Ng’ang’a wa Kenya. ‘Mapepo’ yalimzidi nguvu.

Ni jambo la kumshukuru Mungu kuona Rose ‘amefufuka’ kwa sababu kipaji kikubwa na cha kipekee kilikuwa kikielekea shimoni.

 

Kwako Rose, mapito uliyopitia ni magumu sana na yanahuzunisha sana kwa watu wanaokutakia mema. Mshukuru Mungu wako kwa kukuinua upya, simama kwa miguu yako na chunga sana usirudie yale mambo yaliyofanya ukawa kituko mbele ya jamii.

Bado mashabiki wako wanakuhitaji, bado unao uwezo wa kufanya mambo makubwa kupitia karama uliyopewa na Mungu. Fanya kazi yako kwa nguvu zako zote na Mungu atakubariki. Haleluya!

Comments are closed.