Rostand: Sijaona Straika wa Kunisumbua Simba, Yanga

Kipa raia wa Cameroon anayeidakia African Lyon, Rostand Youthe.

NA WILBERT MOLAND | CHAMPIONI | MAKALA

KIPA raia wa Cameroon anayeidakia African Lyon, Rostand Youthe ni kati ya magolikipa wenye maumbile makubwa kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara. Umbile lake hilo kubwa limeonekana ni tishio kwa washambuliaji wa timu anapokuwa golini kwake akiokoa michomo.

Kipa huyo anayewaniwa vikali na klabu kongwe za Simba, Yanga na Singida United, alijiunga na African Lyon msimu huu wa Ligi Kuu Bara mara baada ya timu hiyo kupanda daraja. Championi Jumatano lilifanya mazungumzo maalum na kipa huyo na kuelezea tetesi za kuwaniwa na klabu hizo kongwe na changamoto anazokabiliana nazo ndani ya African Lyon.

Msambuliaji wa Simba, Shiza kichuya.

UNAJISIKIAJE KUICHEZEA TIMU NDOGO KAMA LYON?

“Binafsi najisikia kuwa na amani k u b wa kuichezea timu ndogo kama hiyo licha ya kukutana na changamoto kadhaa za kibinadamu ambazo ninajitahidi kupambana nazo. “Nikwambie kitu, kuichezea timu ndogo kama hii ya Lyon kunanifanya nicheze kwa amani na kujituma ninapokuwa golini kwangu. “Timu hizi ndogo hazina presha kabisa, tofauti na klabu hizi kubwa za Simba, Yanga na Azam FC zenye mashabiki wengi wanaoweza kukufanya ushindwe kucheza kutokana na kelele zao.”

Mshambuliaji wa klabu ya Yanga Mrundi Hamisi Joselyn Tambwe.

INA MAANA SIMBA NA YANGA ZIKIWEKA OFA NZURI HAUENDI?

“Nikukumbushe moja ya matukio ninayoyakumbuka, la kipa wa zamani wa Simba raia wa Ivory Coast, Vincent Angban yeye alifukuzwa kwenye timu baada ya kufungwa kwenye moja ya mechi muhimu za ligi kuu. “Kiukweli sidhani kama ni sahihi kumfukuza kipa kwa matokeo mabaya ya mechi moja, maamuzi hayo huenda yakawa ya viongozi au mashabiki yaliyochanganyika na presha zao. “Kutokana na mazingira hayo, binafsi ninaona ni bora nikaendelea kupata kipato kidogo Lyon kuliko kwenda sehemu nitakayocheza bila ya kuwa na amani moyoni. “Nashukuru nikiwa hapa Lyon ninapata kipato

kidogo ambacho ninaamini kama ningekuwa Simba au Yanga ningekuwa napata zaidi ya hiki, lakini ninafurahia maisha ya hapa kwani hiki kidogo nashukuru nagawana na familia yangu kwa kuwatumia nyumbani watumie.”

CHANGAMOTO ZIPI UNAZOKUTANA NAZO LYON?

“Zipo nyingi lakini nisingependa kuziweka wazi sana, labda kidogo tu kwenye ulipwaji wa mishahara, ujue Lyon ni timu ndogo ambayo hauwezi kuifananisha na Simba, Yanga ambazo zina mtaji mkubwa wa mashabiki na udhamini. “Nikuhakikishie kuwa, kama Lyon tungekuwa tuna udhamini mkubwa, kwa maana ya wachezaji kulipwa mishahara mizuri, posho na mahitaji mengine, basi tungechukua ubingwa wa ligi kuu. “Kwani ukiangalia uwezo wa
mchezaji mmojammoja ndani ya Lyon ni mkubwa, wa kulinganisha na wachezaji wanaomwagiwa sifa Simba na Yanga.”

Kikosi cha African Lyon.

VIPI TAARIFA ZA KUTAKIWA KUSAJILIWA SIMBA, YANGA?

“Hizo ni tetesi pekee ambazo nimezisikia kutoka kwenye klabu hizo kongwe, pia zipo nyingine za Singida United kunihitaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu. “Wakati tetesi hizo zikiendelea, hakuna timu hata moja iliyonifuata kwa ajili ya mazungumzo, niseme tu kama kuna timu inanihitaji, basi iifuate Lyon kwa ajili ya mazungumzo. “Uzuri ni kwamba mimi mwenyewe mkataba wangu unamalizika mwishoni mwa msimu huu wa ligi kuu.”

MSHAMBULIAJI GANI BORA KWAKO?

“Nimekutana na washambuliaji wengi kwenye msimu huu, labda nikwambie tu sijaona mchezaji wa kunitisha, wote viwango vyao ni vya kawaida, vinafanana. “Unaweza kuniambia Simba, lakini hao wenyewe mechi iliyopita ya ligi kuu walitufunga mabao 2-1 lakini hayo yote tumejifunga wenyewe na hilo lipo wazi kabisa.”

TIMU GANI BORA KWAKO MSIMU HUU WA LIGI KUU?

“Ni timu yangu ya African Lyon ndiyo bora pekee, kama nilivyokwambia mwanzoni kuwa Lyon kama ingekuwa inalipa vizuri mishahara na posho kwa wakati kama zilivyo Simba, Yanga na Azam basi tungechukua ubingwa. “Naendelea kusisitiza kuwa, Lyon ndiyo timu bora kwangu, sema changamoto mbalimbali za nje ya uwanja ndiyo zinasababisha tusionekane bora,” anasema Youthe.


Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment