
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, amesema kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, amevamiwa na watu watatu waliomkanyaga na kumvunja mguu wake wa kulia.
Hayo ameyabainisha mapema leo Juni 9, 2020, wakati akizungumza wanahabari jijini Dodoma na kusema:
“Alfajiri ya leo Juni 9, 2020 tulipokea taarifa kutoka kwa mbunge mwanamke wa Viti Maalum na dereva wa Freeman Mbowe aitwaye Wiliard Urasa (34), ikieleza kuwa Mbowe alikuwa akitokea eneo la Mideri, dereva alimshusha nyumbani wakati akipandisha ngazi kueleka kwenye nyumba yake alikutana na watu watatu wakamshambulia.
“Walielekeza zaidi mashambulizi kwenye mguu wake wa kulia wakimkanyanga kwa mateke, si kwa silaha, sio kwa sime, sio kwa panga….. majeruhi alichukuliwa na kupelekwa hospitali ya Ntyuka DCMC ambapo anaendelea na matibabu.
“Jeshi la polisi linafanya uchunguzi wa kina bila kuacha ukweli wowote katika tukio hili, hili ni tukio kama matukio mengine linachunguzwa na jeshi la polisi, lisitumike kisiasa wala kujiongezea umaarufu.
“Ni marufuku kuingilia uchunguzi wa tukio hili wakati polisi ikiendelea na uchunguzi, tutawahoji walinzi wa eneo lile na majirani ili kupata ukweli wa tukio hili.”
Mbowe ameshambuliwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake jijini Dodoma usiku wa kuamkia leo Juni 9,2020.
Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema iliyotolewa kwenye akaunti ya chama hicho ya Twitter, iliyothibitishwa na Msemaji wa Chama hicho, Tumaini Makene, Mbowe amekimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu na kwamba taarifa zaidi itatolewa na Chama hicho baadaye.

